AFCON: Algeria ndio mabingwa wa bara Afrika

algeria
algeria
Algeria ndio washindi wa kipute cha AFCON mwaka wa 2019 baada ya kuwashinda Senegal 1-0 jijini Cairo.

Senegal ambao hawajawahi kushinda kipute hicho walipewa penalty kunako kipindi cha pili kwa mpira wa mkono lakini ikakataliwa na VAR.

Wachezaji wa Senegal walibubujikwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho. Sadio Mane wa Liverpool alionekana mwenye huzuni Algeria walipokua wakisherehekea ushindi wao.

Senegal ambao walikua wakishiriki fainali hio kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2002 walitawala mechi hiyo lakini wakashindwa kufunga.

Kwingineko, meneja wa Inter Milan Antonio Conte anasema Romelu Lukaku ataboresha kikosi chake lakini akakiri kwamba kuna masuala yanayomzuia kumsajiji mshambulizi huyo kutoka Manchester United.

Inter wanamtaka mbelgiji huyo lakini hawajafikia thamani ya United kwa mchezaji huyo, waliyemsajili kwa pauni milioni 75 kutoka Everton miaka miwili iliyopita. Hatachezea United dhidi ya Inter huko Singapore.

Tukisalia Uingereza, kocha wa Arsenal Unai Emery amekiri kwamba mlinzi Laurent Koscielny huenda akaondoka klabuni humo. Raia huyo wa Ufaransa alidinda kujinga na Gunners katika ziara yao ya kabla ya kuanza kwa msimu nchini Marekani na anataka kuruhusiwa kuregea Ufaransa.

Kuondoka kwake kutawacha pengo la uongozi lakini Emery anasema anaona mlinzi Rob Holding kama anaweza kuwa nahodha.

Tukirejea humu nchini, msururu wa raga wa National Sevens unaanza hii leo mjini Kakamega.

Mabingwa Homeboyz watakua wanatafuta kuonyesha ubabe wao watakapofungua kampeni yao dhidi ya wenyeji Western Bulls wakifuatiwa na mechi kati ya Menengai Oilers na Impala. Mwamba wako katika kundi B pamoja  na Nondies, Mean Machine na Kisumu.

Katika kundi C, KCB watachuana na Kisii, Masinde Muliro na Kabra Sugar. Kenya Harlequins wako katika kundi D wakichuana na Nakuru, Strathmore Leos na chuo kikuu cha Egerton.