YouTube yawinda Ndovu Kuu! Kibao cha Krispah chatolewa Youtube baada ya kuripotiwa

Ngoma hiyo ya msanii Krispar almaarufu kama Ndovu Kuu akishirikisha Khaligraph Jones na Boutrous Munene iliondolewa siku ya Jumapili kwa madai ya suala la hatimiliki.

Muhtasari

•Kulingana na walalamishi, wimbo huo ambao kufikia kuondolewa kwake ulikuwa umetazamwa na zaidi ya watu milioni tatu na nusu pia unadaiwa kuharibia jina chuo kikuu cha Kenyatta.

•Msanii kwa jina Dexta Briyanka anayeaminika kuripoti kibao hicho kwa watawala wa YouTube alidai kuwa Krispah alitumia mdundo wa ngoma yake kutengeneza kibao Ndovu ni Kuu.

Image: YOUTUBE

Kibao 'Ndovu ni kuu' ambacho kimekuwa kikivuma sana  nchini kimeondolewa kutoka mtandao wa YouTube.

Ngoma hiyo ya msanii Krispar almaarufu kama Ndovu Kuu akishirikisha Khaligraph Jones na Boutrous Munene iliondolewa siku  ya Jumapili  kwa madai ya suala la hatimiliki.

Kulingana na walalamishi, wimbo huo ambao kufikia kuondolewa kwake ulikuwa umetazamwa na zaidi ya watu milioni tatu na nusu pia unadaiwa kuharibia jina chuo kikuu cha Kenyatta.

Msanii kwa jina Dexta Briyanka anayeaminika kuripoti kibao hicho kwa watawala wa YouTube alidai kuwa Krispah alitumia mdundo wa ngoma yake kutengeneza kibao Ndovu ni Kuu.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dexta pia alidai kuwa kibao hicho kilikuwa kinachochea vurugu katika chuo kikuu cha Kenyatta.

"Nimeitoa YouTube kwa sababu inakiuka haki zangu na pia inachochea vurugu katika chuo kikuu cha Kenyatta. Hata mzazi halipi karo juu wanasema hakuna masomo KU. Wacha tupatane kortini ikiwa una shida" Dexta aliandika.

Krispah kwa upande wake alikanusha madai ya kutumia mdundo wa Dexter na kudai kuwa ngoma yake haina uhusiano wowote na kibao kinachodaiwa kuwa cha asili.

Alimkashifu vikali msanii huyo aliyemripoti na kumwambia kuwa angempeleka mahakamani.

Ndovu kuu pia alitetea ngoma yake dhidi ya madai ya kuharibia chuo cha Kenyatta jina kwa kusema kuwa kifupisho KU chaweza kumaanisha chochote huku akitoa mifano ya Kabianga University, Karatina University, Kisii Univesity, Kenyan University, kukula ugali na kula ulale.

Kwenye mazungumzo ya simu kati ya usimamizi wa Ndovu Kuu na msanii huyo, Dexter alidai kuwa yeye ni balozi wa chuo cha Kenyatta.