'Hamna haja kutoa taarifa kuhusu yaliyo wazi' Juliani avunja kimya kuhusu madai kuwa anachumbia aliyekuwa mke wa gavana Mutua

Muhtasari

•Picha kadhaa  za msanii huyo akijivinjari na Lilian zimekuwa zikienezwa mitandaoni na kusemekana kuwa wamejitosa kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NG'ANG'A

Mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani hatimaye amejitokeza kuzungumzia madai kuwa anachumbia aliyekuwa mke wa gavana Alfred Mutua Bi Lilian Ng'ang'a.

Tangu Mutua na Lilian watangaze kuvunjika kwa ndoa yao mwezi uliopita uvumi  umekuwa ukitanda mitandaoni kuwa msanii huyo ndiye sababu kuu ya kutengana kwao.

Picha kadhaa  za msanii huyo akijivinjari na Lilian zimekuwa zikienezwa mitandaoni na kusemekana kuwa wamejitosa kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, msanii huyo amechapisha ujumbe wa kimafumbo na kusema kuwa watu wana uhuru wa kufikiria wanavyotaka.

Baba huyo wa mtoto mmoja aliyepata na aliyekuwa mpenzi wake mwigizaji Brenda Wairimu amesema kuwa hakuna haja yake kutoa taarifa kuhusu jambo ambalo ni wazi.

"Asante sana kwa wale ambao wamewasiliana nami ndani ya kipindi cha wiki chache zilizopita. Mola awazidishie.

Hakuna haja ya kutoa taarifa kuhusu suala ambalo ni wazi. Najua mnaweza jiwazia wenyewe. Pateni hitimisho wenyewe. Nawaaminia" Juliani ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.