"Tutaendelea kuwa marafiki" Gavana Alfred Mutua na Lilian Ng'ang'a watangaza kuvunjika kwa ndoa yao

Mutua amemsifia sana Lilian kwa wakati wamekuwa pamoja na kusema kuwa ataendelea kupokea mawaidha kutoka kwake.

Muhtasari

•Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wawili hao wamesema kuwa walifanya maamuzi ya kutamatisha uhusiano wao miezi miwili iliyopita

•Hata hivyo gavana Mutua amesema kuwa hawana ugomvi wowote kwa sasa na wataendelea kuwa marafiki hata baada yankila mmoja wao kuenda njia tofauti.

•Mutua amesema kuwa alifurahia wakati walikuwa pamoja na kumshukuru Mungu kwa kumleta Lilian maishani mwake.

Image: INSTAGRAM//GOVERNOR ALFRED MUTUA

Gavana wa Machakos Alfred Mutua na mke wake Lilian Ng'anga wametangaza kuvunjika kwa ndoa yao.

Kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii wawili hao wamesema kuwa walifanya maamuzi ya kutamatisha uhusiano wao miezi miwili iliyopita.

Gavana Mutua alimtangaza Lilian kama  'First Lady' wa kaunti ya Machakos alipochaguliwa ofisini mwaka wa 2013, nafasi ambayo imewachwa wazi kwa sasa baada ya kutengana kwao.

Hata hivyo gavana Mutua amesema kuwa hawana ugomvi wowote kwa sasa na wataendelea kuwa marafiki hata baada yankila mmoja wao kuenda njia tofauti.

"Lilian na mimi tumekuwa baraka kwa kila mmoja wetu. Miezi  miwili iliyopita, tuliamua kutengana polepole. Tuko katika hali ya amani na tunabaki kuwa marafiki. Tutaendelea kukutana na kubadilishana mawazo mara kwa mara" Gavana Mutua aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mutua amemsifia sana Lilian kwa wakati wamekuwa pamoja  na kusema kuwa ataendelea kupokea mawaidha kutoka kwake.

"Lilian amekuwa 'First Lady' mzuri zaidi na hata kama atafanya miradi mingine chini ya Lilian Nganga Foundation, tumekubaliana kuwa anaweza kuendelea na miradi yake ya kaunti. Atakuwa mshauri wangu ninapoendelea kuongoza kaunti na ninapowania urais kwani naamini mawazo yako na moyo wake. Amekuwa shabiki wangu nambari moja. Mapenzi yetu ni ya kudumu ila nadhani kwa wakati mwingine nafasi na mwelekeo mpya ni muhimu" Mutua alisema.

Mutua amesema kuwa alifurahia wakati walikuwa pamoja na kumshukuru Mungu kwa kumleta Lilian maishani mwake.

"Tunafurahia maisha na tumefikia maamuzi haya kama watu wazima na tukakubaliana. Mimi ni mtu aliyebarikiwa na mwenye furaha na tumekubaliana kulinda na kuungana mkono" Gavana huyo alimalizia kwa kusema.

Bi Lilian amesema walikuwa na wakati mzuri kwenye ndoa  ila alifanya maamuzi kutamatisha uhusiano wao. Alisisitiza kuwa wataendelea kuwa marafiki licha ya kutengana.

"Mipango ya Mungu huwa ya manufaa kwetu. Usiwahi tilia haka ama kuuliza maswali" Alisema Lilian.

Kabla ya kufunga ndoa na Lilian, gavana Mutua alikuwa na mke mwingine aliyefahamika kama Josephine Thitu Maundu ila wakatengana wakiwa na watoto watatu.