Hongera! Mchekeshaji Mulamwah na mpenzi wake wabarikiwa na mtoto wa kike

Muhtasari

•Wawili hao walitangaza kuzaliwa kwa binti yao ambaye wamempatia jina Keilah Oyando kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

•Mapema mwaka uliopita ndoto ya wawili hao ya kufanya familia yao iwe kubwa ilikuwa imefifia baada ya ujauzito ambao Bi Carol alikuwa amebeba kuharibika.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah na mpenzi wake Caroline Muthoni wamekaribisha mtoto wao wa kwanza duniani.

Wawili hao walitangaza kuzaliwa kwa binti yao ambaye wamempatia jina Keilah Oyando kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii.

"Na ni msichana. Muujiza umewasili.. maneno hayaweza kueleza ninavyohisi, ni kitu cha maana zaidi kuwahi fanyika maishani mwangu. Karibu kipenzi @keilah_oyando" Mulamwah aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Msanii huyo ambaye pia ni muuguzi alichukua  nafasi ile kumshukuru mpenzi wake na kumbubujikia sifa kufuatia hatua hiyo.

"Asante mpenzi @carrol_sonie kwa zawadi nzuri. Wewe ni mwanamke jasiri kuweza kufanya haya licha ya yale yote tumepitia. Asante sana kwa waliotutakia mema na kutuombea. Asanteni sana" Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo ameeleza raha kubwa  iliyo moyoni mwake baada ya kubarikiwa na mtoto wake wa kwanza  na amedai kwamba siku itimiapo ataonyesha urembo wa bintiye hadharani.

"Ni mrembo, siwezi subiri kuonyesha walimwengu siku moja na niwe na mazungumzo ya baba na binti. Mimi ni baba mwenye raha. Shukran kwa Mungu" Alisema Mulamwah.

Bi Caroline kwa upande wake ameapa kwamba atampatia bintiye malezi bora zaidi.

"Staa amezaliwa.. nakaribisha kito cha thamani zaidi kwa familia yetu @keilah_oyando. Siwezi subiri kukupa malezi bora" Carol aliandika.

Mapema mwaka uliopita ndoto ya wawili hao ya kufanya familia yao iwe kubwa ilikuwa imefifia baada ya ujauzito ambao Bi Carol alikuwa amebeba kuharibika.