King Kaka azungumzia hali yake ya afya baada ya kuugua maradhi yaliyofanya apoteze kilo 33

Muhtasari

•Gwiji huyo wa nyimbo za kufoka amewashukuru sana mashabiki ambao wamekuwa wakimuombea na kumtumia jumbe za kumtakia afueni ya haraka.

•Msanii huyo ambaye alikuwa amefichua kuwa alipoteza kilo 33 kufuatia maradhi yaliyomwadhiri kwa miezi mitatu amesema kwamba kwa sasa anaendelea kufuata maagizo ya daktari kuhusiana na lishe.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki mashuhuri nchini Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka ametangaza kwamba ashaondoka hospitali na anaendelea kupata nafuu baada ya kuugua kwa kipindi cha miezi tatu.

Kupitia video ambayo alipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram, gwiji huyo wa nyimbo za kufoka amewashukuru sana mashabiki ambao wamekuwa wakimuombea na kumtumia jumbe za kumtakia afueni ya haraka.

"Asante kwa maombi yenu na jumbe zenu na tusiache mazee. Naendelea kupata nafuu, nishatoka hospitali" King Kaka amesema.

Msanii huyo ambaye alikuwa amefichua kuwa alipoteza kilo 33 kufuatia maradhi yaliyomwadhiri kwa miezi mitatu amesema kwamba kwa sasa anaendelea kufuata maagizo ya daktari kuhusiana na lishe.

Kaka amewahakikishia mashabiki wake kuwa anatazamia kurejea hivi karibuni kuona kwamba anaendelea kupata nafuu.

"Acha nikunywe chai.. saa hii nakula manduma kila baada ya masaa matatu. Nimekuwa nikifuatia maagizo ya daktari kuhusu lishe lakini nitarejea. Lazima tudrop EP, lazima tutoe mangoma" King Kaka amesema.

Mapema mwezi huu mwanamuziki huyo anayetambulika sana kutokana na kibao chake 'Wajinga Nyinyi' alisema kwamba alikuwa amepoteza hisia ya ladha kwa kipindi cha miezi miwili na alikuwa akila matunda na kunywa uji tu.

Kaka alisema kuwa hata nguo alizokuwa anavaa hapo awali hazimtoshei kwa sasa kufuatia kupungua kwa ukubwa wa kiuno chake.