'Namuonea huruma kwa kusema najifanya,'Akothee azungumzia ugonjwa wake na jinsi amekejeliwa

Muhtasari
  • Pia amesema kwamba kuna jamaa wake wa karibu ambaye amekuwa akimkejeli na kusema kwamba anajifanya
Esther Akoth

Mwanamuziki mashuhuri Esther Akoth almaarufu kama Akothee amewasuta wanaokosoa mabadiliko ambayo yamejitokeza mwilini wake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano amesema anaonekana mnene kutokana na uvimbe uliosababishwa na hali ya afya ambayo imemwathiri kwa muda sasa.

Akothee amesema maumivu ambayo amekuwa akipata mwilini yamemfanya kukosa usingizi kiasi cha kwamba amekuwa akihofia kuingia kitandani.

Pia amesema kwamba kuna jamaa wake wa karibu ambaye amekuwa akimkejeli na kusema kwamba anajifanya.

'Usikutane na kuanza kuniambia jinsi nilivyo mnene, nina hali ya kiafya, nimevimba kutokana na kuhangaika na maumivu ya kukosa usingizi, naogopa kwenda kulala maana ninaamka na ganzi kwenye vidole vyangu, hali hii inanitisha. Namuonea huruma jamaa yangu mmoja wa karibu aliyesema najifanya  bado sijui nimwambie nini " Akothee amesema.

Msanii huyo amesema kwamba hayuko kwenye shule la bweni ambapo anafaa kuhitisha ruhusa baada ya kuwa mgonjwa.

Akothee ameonekana akishinda kila changamoto maishani mwake kama 'single mother' licha ya kupokea kejeli kutoka kwenye mitandao ya kijamii.

Ni mwanamuziki ambaye amekuwa akiwasaidia wanyonge nchini na ata kuwasomesha watoto ambao hawajiwezi.

"Kwani niko shule ya bweni nahitaji ruhusa ya kwenda nyumbani ? ! Au hata mimi namhurumia nani? Je, mimi ni mfanyakazi, ninaweza kupata muda wa kupumzika na familia yangu na kutoenda kazini  Wao! kama kuna yeyote anayekutakia mabaya ni watu unaowaweka karibu na moyo wako, waombee hata hivyo."