"Alipofariki nilisema nimepoteza baba mwingine!" Jacky Vike 'Awinja' amkumbuka marehemu Papa Shirandula

Muhtasari

•Jacky alimlimbikizia marehemu sifa kochokocho na kukiri alifanya mchango mkubwa zaidi katika mafanikio makubwa ambayo ameweza kupata katika taaluma yake ya uigizaji kufikia sana.

•Malkia huyo ambaye aliigiza kama binti ya Papa Shirandula alisema alimchukulia marehemu kama baba yake tu hata nje ya uigizaji.

•Alisema marehemu alikuwa mwenye kujali sana na alipendelea kumfuatilia kuhakikisha kuwa  anaendelea vizuri kila wakati. 

Jacky Vike na marehemu Papa Shirandula
Jacky Vike na marehemu Papa Shirandula
Image: HISANI

Mwigizaji Jacky  Vike anayefahamika kama 'Awinja' kutokana na jukumu lake katika kipindi cha Papa Shirandula amefunguka kuhusu aliyopitia akiigiza  katika kipindi hicho na uhusiano wake na mwigizaji mkuu pale marehemu Charles Bukeko (Papa Shirandula).

Akiwa kwenye mahojiano katika kipindi cha Churchill Show ambapo alisimulia kuhusu maisha yake, Jacky alisema ana mengi ya kukumbuka na kujivunia kuhusu marehemu Papa Shirandula.

Jacky alimlimbikizia marehemu sifa kochokocho na kukiri alifanya mchango mkubwa zaidi katika mafanikio makubwa ambayo ameweza kupata katika taaluma yake ya uigizaji kufikia sana.

"Charles Bukeko, Papa. Namkumbuka na vitu mingi sana . Nina deni kubwa kwake kufuatia mafanikio yangu. Nilifanya kazi na gwiji. Alikuwa na utaalamu mkubwa sana. Kila alichofanya alikuwa mtaalamu sana na mwenye nidhamu katika eneo la uigizaji. Aliweka muda. Hayo ni mambo ambayo yamenisaidia sana katika sekta ya uigizaji, yale yote nilijifunza kutoka kwake " Alisema Jacky.

Malkia huyo ambaye aliigiza kama binti ya Papa Shirandula alisema alimchukulia marehemu kama baba yake tu hata nje ya uigizaji.

Alisema marehemu alikuwa mwenye kujali sana na alipendelea kumfuatilia kuhakikisha kuwa  anaendelea vizuri kila wakati. 

"Alikuwa mwenye kujali sana. Hata nje ya uigizaji alikuwa anajali sana. Hata ukirudi kazini alikuwa anauliza wikendi imekuwaje  na ananiambia nisikubali kudanganywa na wavulana. Alikuwa baba yetu. Ata alipofariki nilisema nimepoteza baba mwingine baada ya babangu mzazi" Jacky alisema.

Mwigizaji huyo alisema jukumu lake katika kipindi cha Papa Shirandula ndilo ngumu zaidi amewahi kufanya katika maisha yake ya uigizaji kwani alipokuwa anaanza hakuwa na lafudhi ile ya 'Kiluhya'.