Mahakama yaamuru Diana Marua kufuta video ya madai ya ubakaji ya Willy Paul aliyopakia YouTube

Muhtasari

•Amri hiyo ya mahakama inamtaka Diana Marua kufuta video ambayo alipakia YouTube mnamo Desemba 9 kwani madai yake yameathiri kazi na afya ya Willy Paul.

Willy Paul na Diana Marua
Willy Paul na Diana Marua
Image: INSTAGRAM

Mahakama ya Milimani imemuamuru Diana Marua kufuta video aliyotengeneza akidai kuwa mwanamuziki Willy Paul alijaribu kumbaka.

Siku ya Jumatano kwenye ukurasa wake wa Instagram Willy Paul alichapisha picha ya karatasi ya amri za mahakama iliyotiwa saini na hakimu mkuu mwandamizi D.W Mburu huku akionekana kusherehekea ushindi.

Amri hiyo ya mahakama inamtaka Diana Marua kufuta video ambayo alipakia YouTube mnamo Desemba 9 ikielezwa kuwa madai yake yameathiri kazi na afya ya Willy Paul.

"Inaamriwa kuwa video ya mshtakiwa/mlalamikiwa na chapisho la mitandao ya kijamii lililochapishwa kwenye chaneli yake ya YouTube yenye jina la 'My Untold Story, Willy Paul tried to rape me', lfutwe ikusubiriwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi yake kwa vile linamuathiri mlalamishi, kumfanya apoteze fursa za biashara na kumfanya ateseke kiafya" Karatasi hiyo ilisoma.

Mahakama pia imemtahadharisha rapa huyo chipukizi na washirika wake dhidi ya kumharibia jina Willy Paul ikisubiriwa kusikilizwa kwa kesi aliyowasilisha mahakamani.

Onyo kali imetolewa kwa yeyote atakayekaidi amri hiyo ya mahakama ambayo ilitolewa tarehe 29 Desemba.

"Inaamuriwa kuwa mshtakiwa/mlalamikiwa aidha yeye mwenyewe, watumishi wake, wakala, au mtu mwingine yeyote anayeeneza video au kusambaza video hiyo anazuiliwa kwa amri ya muda ya dhuluma ya mahakama dhidi ya kukashifu, kueneza na kuendelea kumharibia jina mlalamishi ikisubiriwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi" Amri ilisema.

Willy Paul aliwasilisha kesi mahakamani mnamo Desemba 12 kufuatia madai ya Diana Marua kwamba aliwahi kujaribu kumbaka miaka kadhaa iliyopita.

Diana Marua ambaye alionekana kawezwa na hisia alipokuwa anatoa madai dhidi ya Willy Paul alisema mwanamuziki huyo alijaribu kujilazimisha kwake ila akaweza kujiokoa.