Jamii ya wakanamungu Kenya yatoa ahadi za kuvutia wanachama zaidi

Muhtasari

• Muungano huo umesema ili mtu ahitimu kuwa mwanachama lazima awe raia wa Kenya miaka 18 na ambaye ana fikra huru na anajitambulisha kama mkanamungu.

• Iwapo mwanachama ataugua ama kufariki muungano huo utatoa mchango wa shilingi 20, 000 kwa familia ili kusaidia katika gharama ya matibabu au mazishi.

• Wanachama wake watapewa kipaumbele kwa ufadhili, udhamini na mafunzo ambayo yataandaliwa kwa ushirikiano na mashirika mengine.

Image: ATHEISTSINKENYA.ORG

Muungano wa wasioamini Mungu nchini Kenya (Atheists in Kenya Society) umetoa maelezo ya jinsi ya kujiunga nao pamoja na manufaa ya kuwa mwanachama.

Kupitia kwa tangazo lililochapishwa katika tovuti yao rasmi,  muungano huo umesema ili mtu ahitimu kuwa mwanachama lazima awe raia wa Kenya aliyehitimu umri wa miaka 18 na ambaye ana fikra huru na anajitambulisha kama kafiri.

Kila mwanachama atahitajika kutoa ada ya shilingi mia tano kila mwaka pamoja na mchango wa shilingi mia moja wakati mmoja wao anapougua ama kuaga dunia.

"Ili kujiandikisha lazima uwe raia wa Kenya zaidi ya umri wa miaka 18 ambaye anajitambulisha kama mtu asiyeamini Mungu, asiyeamini kwamba kuna Mungu, mwenye fikra huru, mwanabinadamu au mtilia shaka. Wanachama wote waliosajiliwa watahitajika kuchanga shilingi 100 kwa ajili ya gharama za mazishi na gharama za matibabu ya wanachama walioathirika" Muungano huo umesema.

Muungano huo vileville umesema kutakuwa na manufaa kochokocho kwa kila mwanachama wake.

Iwapo mwanachama ataugua ama kufariki muungano huo utatoa mchango wa shilingi 20, 000 kwa familia ili kusaidia katika gharama ya matibabu au mazishi.

Muungano huo pia utatoa zawadi kwa wanachama wake ambao wanasherehekea siku ya kuzaliwa, wanaofunga ndoa pamoja na watakaobarikiwa na m/watoto.

"Jumuiya itawasaidia wanachama na familia zao za karibu (mke na watoto) kama ifuatavyo; gharama za matibabu- Ksh 20, 000/ gharama za mazishi Ksh 20, 000. Wanachama wanaweza kuomba usaidizi wa kisheria katika hali ambapo wanabaguliwa au kuandika wosia (ikiwa unapendelea kuchomwa moto baada ya kifo). Wakati wa harusi, siku za kuzaliwa na baby shower tutasherehekea na washiriki kwa njia ya kutoa zawadi na wakati mwingine kuwa sehemu ya sherehe" Muungano huo umesema.

Muungano huo pia umesema wanachama wake watapewa kipaumbele katika ufadhili, udhamini na mafunzo ambayo yataandaliwa kwa ushirikiano na mashirika mengine.