"Kuchelewa kuoa hakukufanyi kijana, inamaanisha umefeli" mbunge Sankok ahimiza watu kuoa wakiwa wadogo

Muhtasari

•Sankok ameshauri watu kuoa mapema wakiwa wangali vijana huku akieleza kuwa kubalehe ni ishara ya Mungu kwamba mtu ako tayari kwa ndoa.

•Amefichua kuwa alifunga pingu za maisha na mkewe alipokuwa anasoma katika chuo kikuu cha Nairobi (UON)  

Image: FACEBOOK// DAVID OLE SANKOK

Mbunge wa kuteuliwa David Ole Sankok amewasuta watu wanaochagua kufunga ndoa wakiwa na umri mkubwa zaidi wa kutoka 40 na kuwakejeli waliooa mapema.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Sankok amesema kitendo cha kuchelewa kuoa hakifanyi mtu kuwa kijana ila badala yake kinamaanisha mtu amefeli.

Isitoshe, mbunge huyo pia amewakosoa wale wanaongoja hadi wakaribie kukoma hedhi ili watulie katika ndoa pamoja na wanaojipondoa ili waonekane wadogo kuliko umri wao halisi.

"Kwa sababu ulichelewa kuoa (ukiwa na miaka 40) haikufanyi kuwa kijana badala yake inamaanisha umefeli. Kwa sababu umetumia vipodozi kuficha mikunjo yako haikufanyi kuwa kijana, Inakufanya kifaa kilichotumika au gari lililofanyiwa ukarabati. Kuolewa ukiwa umekaribia kukoma kwa hedhi badaa ya ukiwa kijana hakukufanyi kuwa mdogo badala yake inakufanya kuwa kahaba aliyejificha na hakuna  tofauti na kahaba anayefanya kazi ya umma. Kwa sababu ulikaa jikoni kwa mama yako muda mrefu kuliko sisi haikufanyi kuwa kijana badala yake inakufanya uwe ombaomba kitaaluma" Sankok alisema.

Mwanasiasa huyo ambaye alifunga ndoa akiwa na  umri mdogo wa miaka 21 amewakosoa sana  wale ambao wanaoa wakiwa wamechelewa kisha kuwaita watu wa rika yao waliooa wakiwa vijana wazee.

Kufuatia hayo, Sankok ameshauri watu kuoa mapema wakiwa wangali vijana huku akieleza kuwa kubalehe ni ishara ya Mungu kwamba mtu ako tayari kwa ndoa.

"Kueni na muache kutuita sisi tuliooa wazee wenu ilhali tuko kwenye mabano ya umri sawa, Kueni na muache walio vijana (kwa umri) kuchukua nafasi zao zinazostahiki. Tunawatumia kama mfano mbaya tunaposhauri watoto wetu. Kumbuka kubalehe ni ishara ya Mungu kwamba unajiandaa kwa ndoa. Zana zote za matumizi ya biashara katika ndoa hukua na kuwa tayari wakati wa kubalehe, Kwa mfano; Ukuaji wa matiti ni kwa ajili ya kunyonyesha sio kuvutia wanaume tayari kwa usherati" Alisema Sankok.

Mbunge huyo amefichua kuwa alifunga pingu za maisha na mkewe alipokuwa anasoma katika chuo kikuu cha Nairobi (UON)  na kukiri kwamba aliweza kulipa karo yake kwa kunolea watu visu pamoja na kuuza mitumba kabla yake kuchaguliwa kuwa kiongozi wa muungano wa wanafunzi wa SONU.