Baba ya Diamond Platnumz awekea mkono ndoa yake na Zuchu

Muhtasari

•Mzee Abdul alisema hatua ya Diamond kuoa itakuwa ya baraka sana kwake na kwa mzazi mwenzake Bi Sunura Kassim almaarufu kama Mama Dangote.

•Aliwashauri wapenzi hao wawe na maelewano mazuri huku akiwakashifu wapingamizi na wakasoaji wa ndoa yao.

Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Image: HISANI

Mzee Abdul Juma ameweka wazi kwamba atakuwa mwenye raha iwapo mwanawe Naseeb Abdul Juma almaarufu kama Diamond Platnumz atafunga ndoa na mwanamuziki mwenzake Zuchu kama inavyoripotiwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Mzee Abdul alieleza kwamba amekuwa akiombea mwanawe sana apate mchumba na aoe.

Mzee Abdul alisema hatua ya Diamond kuoa itakuwa ya baraka sana kwake na kwa mzazi mwenzake Bi Sunura Kassim almaarufu kama Mama Dangote.

"Akifanya suala kama hilo nitashukuru. Nitaona kikiwa kitu cha maana. Akifanya vile wazazi kama wana madhambi watasamehewa. Pindi mtu akioa kuna vipindi unapunguzia wazazi wako madhambi fulani, hivo ndivyo dini yetu inavyokuwa. Akiamua hivo si vibaya maanake Zuchu sio mbaya. Yeye ni msichana mzuri, amefunzwa, anajua utu ni nini. Anafaa kwa kila kitu na ametoka kwa familia nzuri" Mzee Abdul alisema.

Abdul alibariki ndoa iliyopangwa ya mwanawe na Zuchu huku akiwaombea wawili hao kheri njema na baraka tele.

Isitoshe aliwashauri wapenzi hao wawe na maelewano mazuri huku akiwakashifu wapingamizi na wakasoaji wa ndoa yao.

"Naomba mwenyezi Mungu awatie la kheri na baraka, afungue milango ya kheri na neema. Waoane kwa kheri , wakae wote familia mpya iliyokuwa ndani ya ndoa. Ambao wanafikiria tofauti, wanaofikiria sivyo wabaki na huzuni na mshangao  waone kama kweli kitu ambacho hakikuchukuliwa kwa uzito upendeleo umetokea na nyota imetokea kwa mtu fulani na kumefunguliwa neema. Ndoa yao ifanyike na kwa kweli kabisa kusiwe na kigugumizi chochote. Mwenyezi Mungu awaweke wepesi" Mzee Abdul alisema.

Mzee Abdul hata hivyo alikiri hana uhakika kabisa iwapo ni kweli mwanawe na Zuchu wanapanga ndoa kwani kumekuwa na tetesi kubwa kuwa huenda ni kiki tu.