Zuchu atavishwa pete mnamo siku ya Valentines- Mamake Diamond athibitisha

Muhtasari

•Mama Dangote alifichua hayo kupitia mtandao wa Instagram baada ya kuulizwa iwapo ni kweli mwanawe Diamond atakuwa anafunga pingu za maisha na Zuchu.

•Haya yanajiri muda mfupi tu baada ya nyota wa taarabu Khadija Kopa kufichua kwamba tarehe 14 Februari itakuwa siku kubwa kwa binti yake Zuchu.

Diamond Platnumz na Zuchu
Diamond Platnumz na Zuchu
Image: HISANI

Huku tetesi kuwa mastaa wa muziki Diamond Platnumz na Zuchu wanapanga kufunga ndoa katika kipindi cha wiki mbili zijazo, duru za kuaminika zimetaarifu  kwamba kwa kweli jambo kubwa linaenda kutokea Bongo hivi karibuni.

Bi Sanura Kassim almaarufu kama Mama Dangote na ambaye ni mama mzazi wa Diamond amethibitisha kuwa mtunzi wa kibao 'Sukari' Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu atakuwa anavishwa pete mnamo siku ya wapendanao, ukipenda Valentines.

Mama Dangote alifichua hayo kupitia mtandao wa Instagram baada ya kuulizwa iwapo ni kweli mwanawe Diamond atakuwa anafunga pingu za maisha na Zuchu.

"Eti tarehe 14 Zuchu anaoewa Mama Diamond?" Binamu ya Diamond Romy Jones alimuuliza Mama Dangote.

"Anavishwa pete" Mama Dangote alimjibu Jones.

Haya yanajiri muda mfupi tu baada ya nyota wa taarabu Khadija Kopa kufichua kwamba tarehe 14 Februari itakuwa siku kubwa kwa binti yake Zuchu.

Bi Kopa alimtakia bintiye furaha na mafanikio makubwa ifikapo siku ile huku akimhakikishia kwamba ataendelea kuunga mkono maamuzi yake.

"Zuhura mwanangu Nimekulea kwenye maadili na Najua wewe ni binti mwenye maamuzi sahihi na mimi kama Mama yako niseme sina budi kukusapoti .Tarehe 14 inaenda kua siku yako kubwa hakuna mwanamke asie na ndoto hii.M/Mungu akakusimamie najua hutoniangusha .siku hii isiwe tu siku yako kubwa duniani basi pia ikawe ndo mwanzo wa maisha mapya yenye Furaha .M/Mungu Akulinde kiziwanda changu Amin" Bi Kopa aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram

Wanamitandao wameendelea kumwandikia Zuchu jumbe za pongezi na heri njema huku wengi wakibashiri  kuwa atakayekuwa anamvisha pete sio mwingine wala ni Simba mwenyewe, Diamond Platnumz.