"Tafadhali muombeeni!" Size 8 aripotiwa kulazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na maradhi

Muhtasari

•Kanda ya video ambayo ilipakiwa Alhamisi asubuhi ilionyesha msanii huyo akiwa mdhaifu huku wahudumu wawili wa afya wakijitahidi kumzuia asianguke.

Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mhubiri Linet Munyali almaarufu Size 8 Reborn anaendelea kuhudumiwa katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kushambuliwa na ugonjwa usiothibitishwa.

Habari za kulazwa kwa mwanamuziki huyo wa nyimbo za injili zimetangazwa kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kanda ya video ambayo ilipakiwa Alhamisi asubuhi ilionyesha msanii huyo akiwa mdhaifu huku wahudumu wawili wa afya wakijitahidi kumzuia asianguke.

"Size 8 REBORN hatakuwa na mahubiri ya saa saba mchana leo kwa kuwa alilazwa hospitalini, tafadhali muwekeni kwenye maombi yenu na tunaomba kumuona akihubiri mtandaoni hivi karibuni," Tangazo la Instagram lilisoma.

Haya yanajiri takriban miezi mitano baada ya mama huyo wa watoto wawili kupoteza ujauzito wa mtoto wake wa tatu.

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana mwanamuziki huyo alilazimika kufanyiwa upasuaji wa kutoa ujauzito baada ya kukabiliwa na matatizo.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri wameendelea kutakia mke huyo wa DJ Moh afueni ya haraka.