'Najivunia wewe kunifanya babu mdogo,' Mike Sonko amsherehekea bintiye Saumu kwa ujumbe maalum

Muhtasari

•Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimtakia bintiye mema maishani na kumsherehekea kwa kumzalia wajukuu wawili.

•Sonko ambaye hivi majuzi pamoja na familia yake walipigwa marufuku ya kuingia Marekani amemhakikishia bintiye kwamba anampenda sana.

Sonko, bintye Saumu Mbuvi na mjukuu wake
Sonko, bintye Saumu Mbuvi na mjukuu wake
Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Binti wa kwanza wa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko, Saumu Mbuvi, aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Alhamisi.

Sonko ambaye pia ni baba ya mabinti wengine wawili ni miongoni mwa waliosherehekea na Saumu na kumwandikia  ujumbe wa kheri za siku ya kuzaliwa.

Mwanasiasa huyo aliyezingirwa na utata mwingi alimtakia bintiye mema maishani na kumsherehekea kwa kumzalia wajukuu wawili.

"Ninajivunia wewe kwa kunifanya kuwa mmoja wa mababu wadogo zaidi ulimwenguni. Kuwa na ujasiri na endelea kusonga na kufikia yote unayotamani, Kheri ya siku ya kuzaliwa binti yangu mpendwa, uwe na maisha mazuri mbele!" Sonko alimwandikia Saumu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii

Gavana huyo wa zamani ambaye hivi majuzi pamoja na familia yake walipigwa marufuku ya kuingia Marekani amemhakikishia bintiye kwamba anampenda sana.

Saumu ni binti wa Sonko kutoka kwa ndoa yake ya kwanza na  marehemu Janet Njeri ambaye alifariki zaidi ya mwongo mmoja uliopita. 

Alikuwa kwenye ndoa isiyofaulu na seneta wa Lamu, Anwar Loitiptip, na kupata naye watoto wawili.