Rev Victor Githu afunguka jinsi unyanyasaji wa mtandaoni dhidi yake ulivyomuathiri mamake

Muhtasari

•Victor amesema huwa hatishiki na maneno hasi dhidi yake kwani kwa kawaida huwa hayapatii umakini maoni ya watu.

Image: FACEBOOOK//VICTOR GITHU

Mhubiri mdogo zaidi kuwahi kupata umaarufu mkubwa nchini Kenya, Victor Githu amefichua kuwa manyanyaso ambayo amekumbana nayo mtandaoni yameathiri pakubwa mamake.

Githu ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita ameeleza kwamba kwa kipindi kirefu mamake alikuwa anavunjwa moyo na jumbe za matusi zilizoelekezwa kwake kupitia mitandao ya kijamii.

"Nilimuuliza, mama mbona unalia? Mimi ndio natusiwa, wewe walia kwa nini? Nilielewa ni uchungu wa mama lakini nilimwambia hata dhahabu hupitishwa kwa moto. Nimekubali kuwa mada kwa sababu nipo kileleni," Victor alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Mchungaji huyo mwenye umri wa miaka 12 hata hivyo ameweka wazi kwamba alizungumza na mamake na kwa sasa tayari ameweza kuyafungia matusi yanayoelekezwa kwake. 

"Siku hizi mama halii. Tukizungumza naye huwa namwambia nimebarikiwa na ndio maana wananilenga. Mimi nimebarikiwa na nina upendo wa Mungu," Alisema.

Victor amesema huwa hatishiki na maneno hasi dhidi yake kwani kwa kawaida huwa hayapatii umakini maoni ya watu.