Harmonize asherehekea uhusiano wa miaka mitano na meneja Jembe

"Miaka 5 chini nabado tunatabasamu pamoja, sio rahisi," alisema.

Muhtasari

•Jembe, ambaye kitaaluma ni daktari ni meneja wa Harmonize na Mtendaji Mkuu wa Muziki katika Kondegang

•Harmonize alibainisha kuwa si urafiki mwingi  ambao hudumu kwa muda mrefu kama huo hasa pale ambapo pesa na umaarufu vinahusika.

Jembe ni Jembe na Harmonize
Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amesherehekea safari yake ya urafiki wa miaka mitano na meneja  Dkt Sebastian Ndege almaarufu Jembe ni Jembe.

Jembe, ambaye kitaaluma ni daktari ni meneja wa Harmonize na Mtendaji Mkuu wa Muziki katika Kondegang. Pia anamiliki kituo cha habari na hoteli nchini Tanzania.

Siku ya Ijumaa, Harmonize na Jembe walishiriki muda pamoja wakicheza gofu na kufanya mazungumzo ambayo hayajafichuliwa.

"Ni siku nzuri, ya kuburudisha na afya, mazungumzo mazuri na jamaa wangu @harmonize_tz," Jembe aliandika kwenye Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na video inayomuonyesha akiwa na  bosi huyo wa Konde Music Worldwide kwenye uwanja wa gofu.

Harmonize pia alichapisha video hiyo kwenye Instastori  ambapo alichukua fursa kusherehekea umbali ambao wametoka pamoja.

"Miaka 5 chini  nabado tunatabasamu pamoja, sio rahisi," alisema.

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa si urafiki mwingi  ambao hudumu kwa muda mrefu kama huo hasa pale ambapo pesa na umaarufu vinahusika.

“Mungu akubariki kaka na mwenzio,” alimwambia.

Siku chache zilizopita, Bw Jembe alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo Harmonize na aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja walimsherehekea.

"Heri ya siku ya kuzaliwa bosi. Nakutakia maisha mema yenye baraka tele, "Kajala alimwandikia meneja huyo kwenye Instagram.

Jembe alimshukuru muigizaji huyo kwa ujumbe wake licha ya yeye na Harmonize kutofautiana mwishoni mwa mwaka jana.

Kajala pia alikuwa meneja mwenza na Jembe katika Kondegang kabla ya mahusiao yake na Harmonize kugonga ukuta