Mulamwah afichua uhusiano halisi na aliyedaiwa kuwa mridhi wa Sonnie, Ruth K

"Rafiki yangu mzuri sana tangu utotoni @ruthk,” alisema.

Muhtasari

•mzazi mwenza huyo wa muigizaji Caroline Muthoni alisema kuwa Ruth amekuwa rafiki yake mkubwa tangu utotoni.

•Baada ya kutengana na Carrol Sonnie mwaka wa 2021, Mulamwah alikuwa amemtambulisha Ruth kama mpenzi wake.

Ruth K na Mulamwah
Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah amesherehekea msanii wake wa kike na rafiki wa karibu Ruth K.

Huku akimsherehekea kupitia ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatano, mzazi mwenza huyo wa muigizaji Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonnie alisema kuwa Ruth amekuwa rafiki yake mkubwa tangu utotoni.

"Rafiki yangu mzuri sana tangu utotoni @ruthk,” aliandika chini ya picha nzuri za mwanamuziki huyo ambayo alizochapisha.

Hata hivyo, mchekeshaji huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu jinsi walivyokutana na jinsi safari yao ya urafiki imekuwa.

Ruth alijibu chapisho la baba huyo wa binti mmoja na alionekana kuunga mkono maelezo ambayo alitoa kwenye picha.

"Tumetoka mbali 😍😍 Kwa miaka mingi mingine ❤," alisema.

Baadhi ya wanamitandao ambao walitoa maoni walisherehekea urafiki wa wasanii hao wawili.Wengine hata hivyo walionyesha wazi kwamba hawakuamini kuwa wamekuwa marafiki wa muda mrefu.

nebulazzkenya Hiyo ni Uwongo Bana.. Watu sio wajinga.😂😂

yycomedian Usiwahi leta malalamishi juu umesema nyi ni marafiki tu.

marysimon1410 leta picha ya utotoni tuamini.

Kwa muda sasa mrefu, Wakenya wamekuwa wakihoji sana kuhusu uhusiano halisi kati ya mchekeshaji huyo na Ruth hasa kutokana na ukaribu wao na matendo yao pamoja kwenye mitandao ya kijamii.

Wawili hao wameonekana kuwa na ukaribu mkubwa tangu Ruth asainiwe katika lebo ya Mulamwah Entertainment. Mara nyingi wameonekana pamoja kwenye hafla maalum na wamekuwa wakiitana 'bestie'.

Baada ya kutengana na Carrol Sonnie mwaka wa 2021, Mulamwah alikuwa amemtambulisha Ruth kama mpenzi wake.

Mnamo mwezi Machi mwaka jana hata hivyo, mchekeshaji huyo alisema hachumbiani na yeyote na akadai kwamba hakuna uhusiano wowote wa kimapenzi kati yake na Ruth kama ilivyokuwa ikiaminika wakati huo.

Wakati huo, alimtambulisha kipusa huyo kama msanii wake mpya katika lebo yake, 'Mulamwah Ent' na kuongeza kwamba hawakuwahi kuwa wapenzi na  hawakuwa na mpango wa kuchumbiana siku za usoni.

"Kusema kweli hatujawahi kuchumbiana , na hatuna nia ya kuchumbiana.Haikueleweka. Kwa upande wangu mimi nabaki single na kuzingatia kazi zangu na miradi mingine iliyo mbele yangu," alisema.