"Kukushika ilikuwa zawadi kubwa zaidi maishani" Diana Marua amsherehekea kifungua mimba wake

Diana libainisha kuwa bintiye amempa masomo muhimu ya maisha kama vile upendo, uvumilivu na bidii.

Muhtasari

•Huku akimsherehekea kifungua mimba wake, Diana alisema kumshika Heaven mikononi kwa mara ya kwanza ilikuwa maalum sana kwake.

•Bahati alimhakikishia bintiye kuhusu malezi bora na kuahidi kumsaidia hadi aweze kutimiza ndoto zake

Diana Marua na bintiye Heaven Bahati
Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Siku ya Jumanne, Februari 14, mtoto wa kwanza wa mwimbaji Bahati na Diana Marua, Heaven Bahati aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Heaven ambaye ni mtoto wa pili wa Bahati  alisherehekea kutimiza miaka 5 huku ulimwengu wote ukiadhimisha siku ya Wapendanao.

Huku akimsherehekea kifungua mimba wake, Diana alisema kumshika Heaven mikononi kwa mara ya kwanza ilikuwa maalum sana kwake.

"Miaka 5 iliyopita, siku kama hii, tunda la kwanza la tumbo langu, Heaven Bahati, lilizaliwa 😍 Kukushika mikononi mwangu ilikuwa zawadi kubwa zaidi ya maisha yangu. Bado siamini kama umefikisha miaka 5 😭🤧," Diana aliandika.

Rapa huyo alibainisha kuwa binti yake amempa masomo muhimu ya maisha kama vile upendo, uvumilivu na bidii.

"Leo (Feb 14), nakusherehekea kwa namna ya pekee kwa sababu ni siku yako ya kuzaliwa. Nakupenda sana na mradi Mungu ataniweka, nitafanya lolote kukufanya uwe na furaha," alimwandikia Heaven.

Mama huyo wa watoto watatu pia alimhakikishia binti yake kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Bahati aliitaja siku ya kuzaliwa ya binti huyo wake wa pili kuwa siku maalum katika maisha yake na mkewe Diana Marua. Alibainisha kuwa mtoto huyo wake ameleta furaha na mabadiliko makubwa katika maisha yao.

"Saa nne na robo asubuhi miaka mitano iliyopita ulijiunga na Ulimwengu wetu na maisha yetu yakabadilika. Umeendelea kuongeza ladha na Furaha katika Familia yetu," alisema mwimbaji huyo.

Baba huyo wa watoto wanne alimhakikishia bintiye kuhusu malezi bora na kuahidi kumsaidia hadi aweze kutimiza ndoto zake.

Aidha alimuombea Heaven maisha marefu na neema ya Mungu katika hatua zote za maisha ambazo atapiga.

Heaven ni mtoto wa kwanza wa wanandoa Bahati na Diana Marua. Bahati hata hivyo ana binti mwingine mkubwa mwenye umri wa miaka saba, Mueni Bahati, ambaye alipata na mpenzi wake wa zamani, Yvette Obura.

Majesty Bahati ni mtoto wao wa pili huku Malkia Bahati ambaye alizaliwa mwaka jana akiwafungia ukurasa wa uzazi kufikia sasa. Wawili hao pia wanamlea Morgan Bahati ambaye alitimiza miaka 13 mwezi Desemba.