Mwimbaji Anjella achorwa tattoo ya Harmonize tumboni (+Picha)

"Kwa ajili ya kaka yangu @harmonize_tz, mwongoza njia❤," Anjella alisema.

Muhtasari

•Anjella alichorwa tattoo ya jina la Harmonize kwenye tumbo kama njia ya kumtambua kwa mchango wake katika taaluma yake ya muziki.

•Anjella ni miongoni mwa watu wengi waliochukua hatua ya kumtakia Harmonize heri ya siku ya kuzaliwa siku ya Jumatano

Harmonize na Anjella
Image: HISANI

Mwimbaji wa Bongofleva Angelina Samson almaarufu Anjella aliyekuwa bosi wake, Harmonize kwa njia ya kipekee.

Siku ya Alhamisi, malkia huyo wa muziki alichukua hatua kubwa ya kuchorwa tattoo ya jina la bosi huyo wake wa zamani kwenye tumbo kama njia ya kumtambua kwa mchango wake katika taaluma yake ya muziki.

"Kwa ajili ya kaka yangu @harmonize_tz, mwongoza njia❤," aliandika chini ya video iliyomwonyesha akichorwa.

Mwanamuziki huyo ambaye aliondoka rasmi katika lebo ya Konde Music Worldwide takriban miezi miwili iliyopita alichorwa tattoo ya jina la bosi huyo wake wa zamani na tarehe yake ya kuzaliwa.

"Harmonize 15.03.199." aliandikwa.

Anjella ni miongoni mwa watu wengi waliochukua hatua ya kumtakia Harmonize heri ya siku ya kuzaliwa siku ya Jumatano. Katika ujumbe wake, malkia huyo wa muziki wa Bongo alimtaja Konde Boy kama kaka yake.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa kaka @harmonize_tz," aliandika kwenye Instastori na kuambatanisha na picha ya mwimbaji huyo.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, Anjella alidaiwa kutofautiana na bosi huyo wake wa zamani katika suala lisilojulikana hadi kupelekea kusitishwa kwa mkataba wake na lebo ya Konde Music Worldwide. 

Harmonize alithibitisha kuwa msanii huyo wake wa zamani  angeondoka Kondegang mnamo mwezi Novemba mwaka jana na akatoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa tayari kuendelea kutoka alikoachia kumsajili.

“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangali nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Nilichoangalia ni ndoto na hasa za mtoto wa kike.

Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu, najua kuna wenye uwezo mkubwa kunizidi, ukizingatia nimeanza juzi. Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza," alisema.

Aidha aliwataka watu kupunguza siasa kuhusu sababu ya kuondoka kwa Anjella na kuweka wazi kuwa hakudai hela zozote kutoka kwake.

Angella alithibitisha kuondoka kwake Kondegang mwanzoni mwa mwaka huu huku akiiga familia hiyo yake ya zamani.