Anjella azika tetesi za ugomvi na aliyekuwa bosi wake, Harmonize

Mwaka jana ziliibuka tetesi kwamba Harmonize alimtunga mimba msanii huyo wake wa zamani.

Muhtasari

•Anjella ni miongoni mwa watu waliochukua hatua ya kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa mwanamuziki huyo.

•Anjella alidaiwa kutofautiana na bosi huyo wake wa zamani katika suala lisilojulikana hadi kupelekea kusitishwa kwa mkataba wake na lebo ya Konde Music Worldwide. 

Anjella na Harmonize
Image: HISANI

Bosi wa Konde Music Worldwide, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa siku ya Jumatano, Machi 15.

Watu wengi wakiwemo mashabiki na watu mashuhuri walimsherehekea staa huyo wa Bongo huku alikitimiza miaka 29.

Aliyekuwa msanii wake, Anjella ni miongoni mwa watu waliochukua hatua ya kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa mwanamuziki huyo. Katika ujumbe wake, malkia huyo wa Bongo alimtaja Konde Boy kama kakake.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa kaka @harmonize_tz," aliandika kwenye Instastori na kuambatanisha na picha ya mwimbaji huyo.

Hatua yake imechukuliwa kuwa thibitisho kwamba hana ugomvi wowote na bosi huyo wake wa zamani licha ya kuondoka Kondegang.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, Anjella alidaiwa kutofautiana na bosi huyo wake wa zamani katika suala lisilojulikana hadi kupelekea kusitishwa kwa mkataba wake na lebo ya Konde Music Worldwide. 

Harmonize alithibitisha kuwa msanii huyo wake wa zamani  angeondoka Kondegang mnamo mwezi Novemba mwaka jana na akatoa wito kwa yeyote ambaye alikuwa tayari kuendelea kutoka alikoachia kumsajili.

“Nilikutana na Anjella akiwa amejikatia tamaa akiwa na ndoto kichwani. Sikujiangali nina kiasi gani, nilijiamini kwa kuwa wapo watu wanaonisapoti bila kuwalipa senti tano basi watasapoti kipaji cha dada Anjella. Nilichoangalia ni ndoto na hasa za mtoto wa kike.

Nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu, najua kuna wenye uwezo mkubwa kunizidi, ukizingatia nimeanza juzi. Kama kunaye anayeweza kumwendelezea kipaji chake ni faraja kwangu, asisite kujitokeza," alisema.

Aidha aliwataka watu kupunguza siasa kuhusu sababu ya kuondoka kwa Anjella na kuweka wazi kuwa hakudai hela zozote kutoka kwake.

Angella alithibitisha kuondoka kwake Kondegang mwanzoni mwa mwaka huu huku akiiga familia hiyo yake ya zamani.