"Kulea mwanangu kumeamsha utoto ndani yangu!" Lilian Nganga afunguka kuhusu malezi

Lilian alibainisha kuwa imefufua baadhi ya mambo ya kitoto aliyofanya miaka ya nyuma.

Muhtasari

•Bi Lilian Nganga amefunguka kuhusu jinsi  kulea mtoto wake wa miezi kadhaa kumekuwa hadi sasa.

•Lilian aliweka wazi kuwa anafurahia sana hatua ya kumlea mwanawe na mambo ambayo imemlazimu kufanya.

Image: INSTAGRAM// LILIAN NGANGA

Mke wa mwimbaji Julius Owino almaaufu Juliani, Lilian Nganga amefunguka kuhusu jinsi  kulea mtoto wake wa miezi kadhaa kumekuwa hadi sasa.

Lilian Nganga na mume wake Juliani walimkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja duniani, Utheri, mnamo mwezi Julai mwaka jana, takriban mwaka mmoja tu baada ya kuyaweka wazi mahusiano yao.

Akizungumzia kuhusu jinsi ulezi wa Utheri umekuwa kwenye ukurasa wake wa Instagram, mke huyo wa zamani wa waziri wa Masuala ya Kigeni Alfred Mutua alibainisha kuwa imefufua baadhi ya mambo ya kitoto aliyofanya miaka ya nyuma.

"Kulea mtoto huyu kumeamsha utoto ulio ndani yangu ambao ulikuwa umesahaulika kwa muda mrefu," Bi Nganga alisema.

Mama huyo wa mvulana mmoja aliweka wazi kuwa anafurahia sana hatua ya kumlea mwanawe na mambo ambayo imemlazimu kufanya.

"Ninaipenda kwa ajili yangu.. kwa ajili yake.. kwa ajili yetu," alisema.

Juliani alifichua kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza na mkewe Lilian Nganga akiwa kwenye mahojiano mapema mwezi Agosti.

Akizungumza na Presenter Ali, mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka alitangaza habari kwamba walipokea zawadi ya mtoto wa kiume siku zilizokuwa zimepita na kuweka wazi jinsi alivyofurahi kuwa baba tena.

 "Nina watoto wawili. Msichana na mvulana. Nilimkaribisha mtoto wa kiume hivi majuzi na Lilian Ng'ang'a," alisema.

Juliani na Lilian walifunga ndoa katika Paradise Lost mnamo Februari 2, 2022, mbele ya familia na marafiki wa karibu.

Orodha ya wageni ilikuwa chini ya watu 50. Ilikuwa wakati huo ambapo Wakenya waligundua Lilian alikuwa anatarajia mtoto.