Inspekta Mwala aomboleza baada ya kufiwa na mwanafamilia

"Tafadhali mtuweke katika maombi yako wakati huu wa majaribu," aliomba.

Muhtasari

•Siku ya Jumanne, Inspekta Mwala alitangaza kwamba dada yake Annah ameaga dunia kutokana na uvimbe wa ubongo.

•Mapema mwaka huu, Mwala alilazimika kujitokeza kukanusha madai ya kwamba amefariki.

Image: FACEBOOK// INSPEKTA MWALA

Muigizaji Davis Mwabili almaarufu Inspekta Mwala yuko katika hali ya kuomboleza.

Siku ya Jumanne, Inspekta Mwala alitangaza kwamba dada yake Annah ameaga dunia kutokana na uvimbe wa ubongo.

"Habari zenu marafiki, Kwa niaba ya familia, ningependa kuwaarifu  kuhusu kifo cha ghafla cha dada yangu Annah ambaye alifariki kutoka na uvimbe wa ubongo," alitangaza kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

Muigizaji huyo aliwaomba mashabiki wake kusimama na familia yake katika kipindi hiki cha maombolezo.

"Tafadhali mtuweke katika maombi yako wakati huu wa majaribu," alisema.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu mashuhuri walimfariji muigizaji huyo na kutuma risala za rambirambi kwa familia.

Hassan Mwana wa Ali: Makiwa.

John De Captain-Kenya: Pole kwa msiba.

MC Benakyu Comedian: Rambirambi zangu kwa familia yote, pole kaka.

Mapema mwaka huu, Mwala alilazimika kujitokeza kukanusha madai ya kwamba amefariki.

Mwala ambaye anajulikana zaidi kutokana na kipindi cha Inspekta Mwala kwenye Citizen TV alilazimika kuweka mambo wazi kuhusu uvumi huo baada ya video iliyodai amekata roho kusambaa  kwenye mitandao ya kijamii.

Mwezi Januari, akaunti ya Tiktok ilichapisha video ya mkusanyo wa picha za mchekeshaji huyo na kudai kuwa alifariki asubuhi hiyo.

“RIP Mwala, amefariki asubuhi ya leo,” maelezo ya video hiyo yalisomeka.

Mwala hata hivyo alijitokeza kulaani mtumizi wa Tiktok aliyechapisha video hiyo na kusema kwamba alichofanya ni kumuua akiwa hai.

Akizungumza na Citizen Digital, mchekeshaji huyo alifichua kuwa tayari alikuwa amechukua hatua ya kisheria na kumshtaki mhusika.

"Mwala bado yuko hai, yeyote aliyetengeneza klipu hiyo atahadhari kwa sababu nimeripoti kwa DCI na haitakuwa nzuri tutakapokutana nao," alisema.

Mchekeshaji huyo mkongwe alibainisha kuwa sio mara ya kwanza kwa habari za uongo kuhusu kifo chake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

" Wakati huu ilikuwa TikTok, mwaka jana ilikuwa Facebook, wakati mwingine Twitter….inahitaji kuacha," Inspekta Mwala alisema.

Mwaka wa 2018, uvumi kwamba Mwala ameaga dunia ulisambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya muigizaji huyo kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani kando ya barabara ya Mombasa.