Kanisa linapaswa kulaani vikali kinachoendelea Kilifi-Daddy Owen

Msanii wa nyimbo za injili Daddy Owen amejitokeza na kushauri makasisi na makanisa kulaani kitendo hicho.

Muhtasari
  • Mhubiri huyo anadaiwa kuwarai wafuasi wake kufunga hadi kufa wakitumai kuwa jambo hilo lingefanya wakutane na Yesu kama alivyowaambia mhubiri wao.

Huku shughuli za kufukua miili katika ardhi ya dhehebu potovu la mshukiwa na muhubiei Paul Mackenzie zikiendelea,watu mashuhuri,wanasiasa, na wanamitandao wamejitokeza na kulaani kitendo hicho.

Msanii wa nyimbo za injili Daddy Owen amejitokeza na kushauri makasisi na makanisa kulaani kitendo hicho.

Owen alituma risala za rambirambi kwa familia za waathiriwa.

"Kanisa na makasisi wajitokeze na kulaani kwa kiwango cha juu chochote kinachotokea Kilifi! Hii ni mbaya, mbaya na mbaya! Napenda kutoa pole kwa familia zote zilizoguswa, Kwa masikitiko ya dhati na maombi ya faraja, naomba MUNGU awafariji katika kipindi hiki cha majonzi na majonzi,"Alisema Owen.

Haya yanajiri huku uchunguzi dhidi ya mhubiri Mackenzi anayedaiwa kuwapotosha watu kwa madai ya dini ukiendelea. Watu 112 wamedaiwa kupotea huku shughuli ya ufukuzi wa miili ya watu wanaodaiwa kufa kutokana na imani potovu ya mhubiri wa Kilifi Paul Mackenzie ikiendelea.

"Tumetengeneza madawati ya ufuatailiaji na ushauri katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi kwa mwitikio wa Shakahola. Kufikia sasa ,watu 112 wameripotiwa kutoweka kutoka kwenye dawati la ufuatiliaji," Red Cross ilisema kupitia ukurasa wao wa Twitter.

Maafisa waliokuwa wakifanya uchunguzi na ufukuzi, siku ya Jumapili tarehe 23 Aprili walichimbua miili 18 zaidi ikifikisha nambari ya ya miili iliyofukuliwa hadi 39.

Familia za waliopotea zimetoa wito kwa serikali kutilia mkazo usakaji wa wale wanaojificha katika msitu wa Shalakola huku maafisa wa uchunguzi wakiendelea kupata makaburi zaidi.

Mhubiri huyo anadaiwa kuwarai wafuasi wake kufunga hadi kufa wakitumai kuwa jambo hilo lingefanya wakutane na Yesu kama alivyowaambia mhubiri wao.