"Najua ungefurahi" Esther Musila atamani mamake angekuwa hai akutane na Guardian Angel

"Najua ungefurahi sana kuniona katika nafasi hii mpya na najua tungekuwa tukiimba nyimbo uzipendazo pamoja," Musila alisema.

Muhtasari

•Huku akimsherehekea mzazi huyo wake siku ya Jumanne, Bi Musila alimtaja marehemu kama nguzo kuu ya maisha yake.

•Musila, 53, alifichua kuwa mama yake alifariki akiwa usingizini, saa chache tu baada ya yeye na kaka yake kumtembelea.

na marehemu mama yake.
Esther Musila na marehemu mama yake.
Image: INSTAGRAM

Mkewe mwimbaji Guardian Angel, Esther Musila amemkumbuka marehemu mamake takriban miaka saba baada ya kuaga dunia.

Huku akimsherehekea mzazi huyo wake siku ya Jumanne, Bi Musila alimtaja marehemu kama nguzo kuu ya maisha yake.

"Ulinifundisha kuthamini kila siku ya maisha yangu na kuishi kana kwamba hakuna kesho. Nililelewa na mwanamke mwenye nguvu na najua kila wakati ulikuwa unasimama nami," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Musila alimuombea mzazi huyo wake mapumziko ya amani na kueleza jinsi anavyojivunia miaka ambayo walishiriki pamoja.

Hata hivyo, alieleza anavyotamani marehemu angekuwa hai ili ashuhudie maendeleo yake na akutane na mumewe Guardian Angel.

"Mama, natamani ungeishi muda mrefu zaidi ili ukutane na mwanaume mzuri zaidi katika maisha yangu sasa. Najua ungefurahi sana kuniona katika nafasi hii mpya na najua tungekuwa tukiimba nyimbo uzipendazo pamoja," alisema.

Aliongeza,"Wajukuu zako pia wamefanya upate fahari kama vile ungetaka wafanye. Endelea kutuangalia sote hadi siku moja tutakapokutana tena. Tunakukumbuka na tunakupenda milele mama."

Musila, 53, alifichua kuwa mama yake alifariki akiwa usingizini, saa chache tu baada ya yeye na kaka yake kumtembelea.

Alitaja siku ambayo mamake alifariki kama siku ya giza zaidi maishani mwake huku akisimulia matukio yaliyofuata.

"Miaka 7 iliyopita, asubuhi kama hii, nilipokea simu kwamba mama yangu mpendwa amefariki usingizini. Hii ilikuwa chini ya saa 12 baada ya mimi na kaka yangu Fred kwenda kijijini kwa wikendi. Ilikuwa siku mbaya zaidi katika maisha yetu."  

"Bado sijui tulipataje nguvu ya kuendesha gari hadi Machakos, kwa kweli ilionekana kama ndoto. Ninaamini kabisa hadi leo kwamba Mwenyezi alilisuluhisha kwa njia yake mwenyewe na alitaka tutumie saa za mwisho za maisha ya mama pamoja naye," alisema.

Esther Musila alizaliwa Machakos yapata miaka 53 iliyopita na yeye ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa na binti pekee wa wazazi wake.