Mr Seed apata alama maalum mwilini kukumbuka siku aliyoponea kifo chupuchupu kufuatia ajali

Mwimbaji huyo alionyesha tattoo ya tarehe ‘29/4/2023’ iliyochorwa kwenye mkono wake wa kushoto.

Muhtasari

• Mr Seed amechorwa tattoo maalum ya kukumbuka siku ambayo alinusurika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

•Mwanamuziki huyo alitumbuiza huku akiwa na mikongojo mikononi kwani viungo vyake bado havijapona kikamilifu.

Image: INSTAGRAM// MR SEED

Mwimbaji Moses Tarus Omondi almaarufu Mr Seed amechorwa tattoo maalum ya kukumbuka siku ambayo alinusurika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

Siku ya Jumanne, mwimbaji huyo wa nyimbo za injili na za mapenzi alionyesha tattoo ya tarehe ‘29/4/2023’ iliyochorwa kwenye mkono wake wa kushoto.

Mr Seed alionyesha video yake akiwa amelala kitandani baada ya kuchorwa tarehe hiyo ambayo ataikumbuka daima.

Mnamo April 29 mwaka huu, msanii huyo wa zamani wa EMB records aliponea kifo chupuchupu baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani kwenye barabara ya Nairobi-Nanyuki. Ajali hiyo ilichukua uhai wa mmoja wa rafiki yake na mwenzake kazini, mpiga video Ambrose Khan ambaye alizikwa mwezi jana.

Marehemu Ambrose alikuwa kwenye gari moja na Mr Seed, DK Kwenye Beat, mpiga picha mwingine na mfanyabiashara wakati wa ajali.Yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa kwa  gari hilo ambaye alipoteza maisha huku wengine wawili waliokuwa kwa gari ambalo waligonga nalo wakifariki dunia pia.

Mr Seed na wenzake walionusurika walipata majeraha mwilini, ambayo mwimbaji huyo wa kibao 'Dawa ya Baridi' bado hajaweza kukabiliana nayo kikamilifu. Hata hivyo amepata maendeleo makubwa kiafya tangu ajali hiyo kutokea.

Wikendi iliyopita, Mr Seed alitumbuiza kwa mara ya kwanza tangu kunusurika katika ajali hiyo. Alikuwa miongoni mwa wasanii ambao walitumbuiza katika Infinity Tavern, mjini Eldoret siku ya Jumamosi.

Mwanamuziki huyo alitumbuiza huku akiwa na mikongojo mikononi kwani viungo vyake bado havijapona kikamilifu.

"Namshukuru Mungu sasa naweza kuendelea kufanya ambacho ninapenda. Hii ni shoo ya kwanza na mashabiki walijitokeza kwa ajili yangu," alisema katika taarifa yake siku ya Jumapili.

Aliambatanisha ujumbe huo na video ya mashabiki wakiwa wamejumuika katika kilabu wakati wa tamasha hilo.