Mr Seed amuomboleza kihisia rafikiye aliyeaga katika ajali iliyomuacha na majeraha mabaya

Mwimbaji huyo alimtaja marehemu kama rafikiye mzuri na mtu mnyenyekevu.

Muhtasari

•Mwimbaji huyo wa kibao 'Dawa ya Baridi' alitumia fursa hiyo kufufua kumbukumbu zake na marehemu mnamo siku ya ajali.

•Alizungumzia jinsi alivyovunjika moyo wakati akimuaga mpiga video huyo ambaye ndiye pekee aliyeaga katika ajali hiyo ya mwezi uliopita.

amemuomboleza rafikiye Ambrose Khan
Mr Seed amemuomboleza rafikiye Ambrose Khan
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za Injili na za mapenzi Moses Omondi almaarufu Mr Seed amemuomboleza rafiki yake na aliyekuwa mwenzake, Ambrose Khan aliyefariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mnamo Aprili 29, 2023.

Akizungumzia ajali hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mr Seed alimtaja marehemu kama rafikiye mzuri na mtu mnyenyekevu.

"29/4/2023 ni siku ambayo sitaisahau maishani mwangu. Nilipoteza kaka, jamaa mmoja mnyenyekevu niliyemfahamu. Mpaka sasa bado siamini. RIP Khan," Seed alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Dawa ya Baridi' alitumia fursa hiyo kufufua kumbukumbu zake na marehemu mnamo siku ya ajali.

"Tulitumia siku nzima na wewe. Tulikuwa na wakati mzuri na tulibadilishana mawazo mengi na mipango ya siku zijazo. Tutakukumbuka sana,"

Katika chapisho jingine, Mr Seed alishiriki picha yake akiwa amesimama kando ya kaburi la Khan mnamo siku ya kuzikwa kwake wiki chache zilizopita ambapo alionekana akiwa amezidiwa sana na hisia.

Alizungumzia jinsi alivyovunjika moyo wakati akimuaga mpiga video huyo ambaye ndiye pekee aliyeaga katika ajali hiyo ya mwezi uliopita.

"Mungu awape amani wanafamilia wako na marafiki zako wote na Mungu awafariji wote wanaokufahamu pia," Seed alisema.

Takriban wiki tatu zilizopita, mwanamuziki huyo wa injili alipambana na majeraha ya mwili na kuhuduhuria mazishi ya Ambrose Khan  nyumbani kwao katika eneo la Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru.

Wakati wa maziko hayo, Mr Seed alionekana akihangaika kusimama na kutembea  alipoombwa kuwasalimia waombolezaji. Pia alionekana akilia kwenye eneo la kaburi la marehemu baada ya kuzikwa shambani mwao.

Baadaye, kwenye ukurasa wake wa Instagram, alipakia picha yake akiwa amesimama kando ya jeneza la Ambrose na kueleza jinsi alivyoumizwa na kufariki kwa mshirika wake wa karibu.

Wakati huohuo, aliwafahamisha mashabiki wake kuwa atachukua mapumziko kutoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda ambao haujawekwa wazi ili kuangazia afya yake ya mwili na ya kiakili.

"Ninatoka kwenye mitandao ya kijamii kwa muda, nahitaji kujishughulisha na afya yangu/akili yangu. Nitarudi hivi karibuni. Baraka. Nawapenda mashabiki wangu, tuonane hivi karibuni," aliandika kwenye Instastori zake.

Marehemu Ambrose alikuwa kwenye gari moja na Mr Seed, DK Kwenye Beat, mpiga picha mwingine na mfanyabiashara wakati wa ajali.Yeye ndiye mtu pekee aliyekuwa kwa  gari hilo ambaye alipoteza maisha huku wengine wawili waliokuwa kwa gari ambalo waligonga nalo wakifariki dunia pia.