Gidi apigwa na butwaa baada ya kuhesabu mamilioni Sauti Sol walivuna kwenye Sol Fest

Sauti Sol walikuwa wamedokeza kwamba tamasha la Jumamosi lingekuwa la mwisho kufanya wakiwa pamoja.

Muhtasari

•Bien, Savara, Chimano na Fancy Fingers walitumbuiza pamoja na Nviri na Bensol katika tamasha lililofanyika Uhuru Gardens Jumamosi jioni.

•Gidi alifanya mahesabu yake na kugundua kuwa waimbaji hao wanaweza kuwa waliingiza zaidi ya milioni 67 siku ya Jumamosi.

amewapongeza Sauti Sol baada ya shoo yao kubwa siku ya Jumamosi.
Gidi amewapongeza Sauti Sol baada ya shoo yao kubwa siku ya Jumamosi.

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi ameipongeza bendi maarufu ya Kenya, Sauti Sol kwa tamasha lao kubwa lililofanyika wikendi.

Siku ya Jumamosi, bendi hiyo ambayo ina wasanii wanne; Bien –Aime Baraza, Savara, Willis Austin Chimano na Fancy Fingers walipiga shoo ya kusisimua katika tamasha la Sol Fest katika bustani ya Uhuru. Inasemekana walikuwa na hadhira ya takriban mashabiki 15,000.

Gidi alifanya mahesabu yake baada ya shoo hiyo na kugundua kuwa waimbaji hao wanne wanaweza kuwa waliingiza zaidi ya milioni 67 kutokana na tamasha hilo lililohudhuriwa na watu wengi.

"Tamasha la Sauti Sol liliripotiwa kuwa na wahudhuriaji 15,000. Walikuwa wakitoza Ksh 4,500. Nimefanya hesabu, wamekusanya milioni 67.5,” Gidi aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mtangazaji huyo mahiri aliambatanisha taarifa yake na picha za hesabu zake kuonyesha jinsi alivyofikia kiasi ambacho Sauti Sol walikusanya.

Pia alibainisha kuwa alihesabu tu kiasi ambacho bendi hiyo ya watu wanne inaweza kuwa ilikusanya kutoka kwa tamasha la mashabiki, bila kuzingatia shoo ya VIP.

“Ile ya VIP sijahesabu. Sasa hii ni pesa nzuri. Kazi ngumu inalipa. Hongera Sauti SOL,” aliandika.

Bien, Savara, Chimano na Fancy Fingers walitumbuiza pamoja na Nviri na Bensol katika tamasha lililofanyika Uhuru Gardens Jumamosi jioni. Tiketi zote zilizokuwa zikiuzwa Sh 4500 tayari zilikuwa zimeshauzwa kabla ya tarehe ya tamasha, hakuna tiketi zilizokuwa zikipatikana getini.

Baada ya tamasha hilo, bendi hiyo ilifichua kuwa takriban mashabiki 15,000 walihudhuria shoo hiyo na kuwashukuru kwa sapoti kubwa.

"Kwa mashabiki wetu wa ajabu, upendo wetu mkuu na sauti! Tunakushukuru sana kwa miaka 20 ya usaidizi wenu usioyumbayumba. Asanteni kwa kufanya @solfestafrica kuwa tamasha kuu katika Afrika Mashariki! 🌟 Tunapochukua mapumziko mafupi, kumbuka, Solfest inaendelea kuishi kwa sababu yako. Endelea kufuatilia kitakachofuata!” Sauti Sol ilisema.

Bendi hiyo yenye vipaji ilikuwa imedokeza hapo awali kwamba tamasha la Jumamosi lingekuwa la mwisho kufanya wakiwa pamoja. Mashabiki hata hivyo wanasubiri kuona hatua yao inayofuata itakuwaje.