DJ Shiti amsuta vikali Mtumishi kwa kumsema vibaya mamake hadharani

Shitti alisema hakupenda kitendo cha mchekeshaji huyo mwenzake na akibainisha kuwa ni kitendo cha kijinga sana.

Muhtasari

•DJ Shitti amemkosoa Mtumishi kuhusu kisa cha hivi majuzi ambapo alisema hadharani mambo mabaya kumhusu mamake.

•Mtumishi alidai kuwa mama yake amekuwa akishiriki uchawi kwa miaka mingi, kitu ambacho alitumia kuvunja familia yake.

amemsuta mchekeshaji mwenzake, Mtumishi
DJ Shiti amemsuta mchekeshaji mwenzake, Mtumishi
Image: HISANI

Mtumbuizaji maarufu wa Kenya Steven Oduor almaarufu DJ Shiti amemkosoa mchekeshaji mwenzake Gilbert Baraza almaarufu Mtumishi kuhusu kisa cha hivi majuzi ambapo alisema hadharani mambo mabaya kumhusu mamake.

Mwezi uliopita, Mtumishi alishangaza taifa nzima baada ya kusimama mbele ya waumini wa kanisa na kuibua shutuma za ushirikina miongoni mwa malalamiko mengine mazito dhidi ya mama yake.

Wakati akizungumza na Chipukeezy kwenye kipindi cha Chipukeezy Show, DJ Shitti alisema hakupenda kitendo cha mwenzake huyo wa zamani kwenye Churchill Show akibainisha kuwa ni kitendo cha kijinga sana.

“Juzi kuna kitendo niliona na sikupenda kabisa. Kuna kijana tulikuwa tunafanya na yeye comedy niliona alienda kwa hizi kanisa ambazo zimekuja siku hizi akapewa mic akaanza kuingilia mama yake mzazi. Kitendo hicho niliona kitendo kama kitendo cha kipumbavu sana,” DJ Shitti alisema.

Muigizaji huyo wa zamani wa Real Househelps of Kawangware alisema kuwa kuna watu wengi wanapitia mambo mengi mabaya wakiwa kimya huku akibainisha kuwa hatua ya Mtumishi kumzungumzia vibaya mzazi wake hadharani haikustahili.

Pia alidai kwamba mambo ambayo mwenzake huyo wa zamani katika Churchill alilalamikia yalikuwa madogo sana ikilinganishwa na mambo ambayo watu wengine wanapambana nayo.

“Ukiangalia vitu ambavyo unalalamikia, ni vitu vya kipumbavu sana.. ukienda mbele ya TV uanze kuchomea mama yako mzazi, watu wamefanyiwa vitu mbaya huku nje. Wazazi wamewafanyia vitu vibaya huku nje na watu wamenyakua. Vitu alikuwa anaongea sio worth pale kuchomea mzazi wake,” alisema Shitti.

Wakati akizungumza katika ibada ya kanisa la Jesus Compassion Ministry katikati mwa mwezi jana, Mtumishi alidai kuwa mama yake amekuwa akishiriki uchawi kwa miaka mingi, kitu ambacho alitumia kuvunja familia yake.

Mchekeshaji huyo alifunguka kuhusu jinsi mamake alivyomhusisha katika shughuli zake za uchawi dhidi ya baba yao akibainisha kuwa mwanamke huyo aliyemzaa hakuwa sahihi kufanya hivyo.

“Mama yangu alivunja boma lake. Kwa nini niseme hivi, alinihusisha kwa mambo ambayo mimi sifai kuhusika. Nikiwa mdogo alikuwa ananipatia dawa za waganga niekee baba yangu kwa mlango ili akija afanye nini… Bila shaka, kila mara mtoto ana hisia na hana hatia , baba yangu akikuja nilikuwa namwambia mama alinipea niweke kitu hapa alafu anatoa inakuwa ni vita kwa nyumba,” Mtumishi aliwaambia washirika.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa ana uchungu sana na mama yake na kubainisha kuwa hata akifa leo, hawezi kumuomboleza kabisa.

“Mimi mama yangu, acha tu niseme ukweli, hata akifa leo, sitahisi chochote. Kwa miaka miwili iliyopita, tangu 2021, sijaongea na yeye,” alisema.

Aidha, alifichua tangu mamake kudaiwa kuvunja ndoa yake mwaka 2021, amekuwa akipuuza simu zake kwani hayuko tayari kuzungumza naye.