Taharuki! Massawe ampatanisha Mtumishi na mamake hewani baada ya kudai ni mshirikina

“Kama alisema mimi ni mchawi, basi akuje atoe hayo manyoka. Kama mimi ni mchawi, hata yeye ni mchawi," Mamake Mtumishi alisema.

Muhtasari

•Massawe alimpigia simu mamake Mtumishi ambaye alisikika kuwa na uchungu sana huku akilalamika kuhusu hatua ya mwanawe kumsema vibaya hadharani.

•Mamake Mtumishi alitupilia mbali madai ya uchawi ambayo mwanawe aliibua akimtaka aende aonyeshe ushahidi kuthibitisha kuwa ni kweli.

Image: RADIO JAMBO

Kipindi cha Alhamisi cha Bustani la Massawe kiligeuka kuwa kikao moto wakati mtangazaji Massawe Japanni alipojaribu kumpatanisha mchekeshaji Gilbert Barasa (Mtumishi) na mama yake mzazi.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show amekuwa akivuma sana kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi cha siku kadhaa zilizopita baada ya kusikika akisema mambo ya kushtua kuhusu mamake wakati wa kipindi cha kanisa siku ya Jumapili.

Katika kipindi cha Alhamisi, Massawe alimpigia simu mamake Mtumishi ambaye alisikika kuwa na uchungu sana moyoni huku akilalamika kuhusu hatua ya mwanawe kumsema vibaya hadharani.

“Kwa nini alinipeleka akaniweka kwa ulimwengu mzima? Sitaki kuongea na yeye saa hii! Kama anataka tuongee, akuje nyumbani tuongee mbele ya watu wetu!” Mama Mtumishi alisema kwa sauti yenye ghadhabu sana.

Pia alionekana kutupilia mbali madai ya uchawi ambayo mwanawe aliibua akimtaka aende aonyeshe ushahidi kuthibitisha kuwa ni kweli.

“Kama alisema mimi ni mchawi, basi akuje atoe hayo manyoka. Kama mimi ni mchawi, hata yeye ni mchawi. Wachana na hizo, sitaki kuongea. Kama ni kuzungumza, ni mbele ya wazazi wangu na ndugu zangu, akuje tuongee, sitaki kuongea sasa,” alisema kisha akakata simu mara moja.

Mtumishi ambaye alikuwa mgeni wetu maalum katika kipindi cha Alhamisi mchana alijitetea akisema kuwa hakuwa amepanga kumwanika wazi mama yake na kudai kuwa ni hisia aliyoipata akiwa kanisani.

“Mimi sikuenda hadharani. Hisia hiyo ilikuja nilipokuwa kwenye madhabahu na nikasema hapa ndipo mahali pazuri. Sio kitu ambacho nilikuwa nimepanga kusema. Niliskia tu imenitoka. Nimeishi nayo tangu nikiwa mtoto,” Mtumishi alisema.

Mtangazaji Massawe Japanni alifanya jaribio la pili la kumpigia simu mamake Mtumishi na mara baada ya kupokea, mchekeshaji huyo alichukua nafasi hiyo kuomba msamaha.

“Mama, naomba msamaha lakini ningependa kujua kama nimewahi kukosea ili niombe msamaha,” Mtumishi alimwambia mama yake kwenye simu.

Mamake Mtumishi ambaye alizungumza kwa sauti tulivu kwenye simu ya pili alisisitiza kwamba wanapaswa kuwa na kikao cha familia ili kutatua mzozo wao.

Mara hii alizungumza vizuri kuhusu mwanaye na kusisitiza kuwa licha ya yote yaliyotokea, bado mchekeshaji huyo ni mtoto wake.

“Kama uliskia uchungu mbona hukuja? Hata bosi yangu amekuja hapa kuniuliza, unataka kuniharibia kazi nani anilishe,” Mama Mtumishi alimuuliza mwanawe.

Aliongeza, “Tutaongea nyumbani, na sio pekee yangu kabisa, na sio mahali kwingine nyumbani. Wewe ni mtoto wangu. Sina shida na wewe.”

Mtumishi alifurahia kuongea vizuri na mamake baada ya muda mrefu na akasema, “Nimefurahi mama amesema tuende tuongee. Hivyo ndo nilikuwa nataka. Simchukii, nampenda ni mama yangu”

Image: RADIO JAMBO