Mtangazaji Gidi amuomboleza mwanahabari Washington Akumu

Gidi alitaja Aprili kuwa mwezi wa huzuni, kuona mwanahabari mwingine, Michael Oyier alifariki siku chache zilizopita.

Muhtasari

•Akumu alifariki hospitalini baada ya kupata mshtuko wa moyo siku ya Jumatatu, Aprili 22, jioni, familia yake na marafiki walisema.

•Alikuwa akielekea kupata ahueni kufuatia msururu wa shughuli katika hospitali ya Nairobi.

Marehemu Washington Akumu
Image: HISANI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi amemuomboleza aliyekuwa mwandishi wa habari za biashara wa Nation na mhariri mkongwe Washington Akumu.

Akumu alifariki hospitalini baada ya kupata mshtuko wa moyo siku ya Jumatatu, Aprili 22, jioni, familia yake na marafiki walisema.

Huku akimuomboleza marehemu Akumu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Gidi alitaja mwezi wa Aprili kuwa wa huzuni, kuona kwamba mwanahabari mwingine, Michael Oyier naye alifariki siku chache zilizopita.

“Hata kabla hatujamzika Michael Oyier, gwiji mwingine wa vyombo vya habari ameanguka, mwezi wa huzuni ulioje. Rest in power Washington Akumu,” Gidi aliandika.

Akumu, ambaye alikuwa mhariri wa biashara katika shirika la Nation Media Group, alikuwa na saratani ya uti wa mgongo na alikuwa akifanyiwa matibabu ya kemikali hadi kifo chake.

Alikuwa akielekea kupata ahueni kufuatia msururu wa shughuli katika hospitali ya Nairobi.

Kulingana na LinkedIn yake aliondoka Nation Media Group mwaka wa 2014 na kujiunga na kampuni ya Redhouse Public Relations ambako alifanya kazi kama Mkurugenzi wa Akaunti ya Kundi.

Mnamo 2016, alijiunga na Media Edge Public Relations kama Mkurugenzi Mkuu, nafasi ambayo alihudumu hadi kifo chake.