“Ukoo uko salama!” Mulamwah ajawa bashasha babake akikutana na mwanawe, amshukuru Ruth K kwa kumzalia

Mchekeshaji huyo alimshukuru mzazi mwenzake kwa ajili ya mtoto wao na pia kumkaribisha nyumbani.

Muhtasari

•Mulamwah alichapisha video ya babake akiwa amemshika mwana wao huku yeye na Ruth K wakitazama na kuzungumza naye.

•Pia alishiriki video nyingine inayoonyesha jinsi babake alivyosisimka baada ya kutembelea nyumbani na gari lake jipya aina ya Mercedes.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah alijawa na furaha baada ya baba yake hatimaye kukutana na mwanawe Oyando Jnr.

Mchekeshaji huyo, mpenzi wake Ruth K pamoja na mtoto wao mchanga hivi majuzi walisafiri hadi Kitale ambapo wamekuwa wakifurahia muda na familia na wenyeji.

Siku ya Jumatano, baba huyo wa watoto wawili alichapisha video ya babake akiwa amemshika mwana wao huku yeye na Ruth K wakitazama na kuzungumza naye.

Katika upande wa maelezo, alimshukuru mzazi mwenzake kwa ajili ya mtoto wao na pia kumkaribisha nyumbani.

“Hatimaye Kalamwah (Oyando Jnr) anakutana na Babu. Ukoo sasa uko salama, asante bestie kwa zawadi hii ya ajabu, karibu nyumbani,” Mulamwah aliandika chini ya video hiyo.

Aliongeza, “baba 2, wana 2. Sote tulingojea wakati huu kwa muda mrefu sana. Mungu ni mkuu. Nina furaha, na nimejaa maisha tena. Team Kitale asanteni sana kwa ukaribisho.

Mchekeshaji huyo pia alishiriki video nyingine inayoonyesha jinsi babake alivyosisimka baada ya kutembelea nyumbani na gari lake jipya aina ya Mercedes.

“Mzee amenice, Mjerumani keshafika mtaa. Ninajivunia kuona baba akiwa na furaha. Mungu ni mkubwa, inawezekana,” alisema chini ya video hiyo.

Mulamwah, Ruth K na mwana wao Oyando Jr walikaribishwa kwa shangwe na nderemo wakati walipozuru nyumbani kwao Kitale, kaunti ya Trans Nzoia mnamo siku ya Jumanne.

Baba huyo wa watoto wawili alichapisha video za wakazi kadhaa, hasa vijana wakiwa na pikipiki wakiwakaribisha kwa shangwe tele huku wakiwa wamebeba matawi wakati alipokuwa akilindesha nyumbani gari lake jipya aina ya Mercedes lililokuwa limebeba familia yake.

Katika video hiyo, baadhi ya vijana walionekana wakikimbia mbele ya gari la Mulamwah, wengine wakifuata nyuma na pembeni huku wengine wakifuata kwa pikipiki huku wakipiga honi.

“Kitale!” Mulamwah aliandika chini ya video hizo na kuisindikiza kwa emoji ya moyo ili kuashiria upendo.

Mpenzi wake, Ruth K pia alionekana kufurahia mapokezi hayo mazuri na akawahakikishia mashabiki wake kwamba angeshiriki video ya kina kuihusu tukio hilo.

Hapo awali, mchekeshaji huyo alikuwa amedokeza kwamba angempeleka mtoto wake mdogo, Oyando Jr nyumbani.

"Kalamwa ufike nyumbani sasa," alisema wikendi na kuambatanisha ujumbe huo na picha yake, mpenziwe na mwanawe katika uwanja wa ndege.