"Anauliza kila wakati mama yuko wapi" Makokha azungumzia mwanawe ,11, kufuatia kifo cha mamake

Alisema kufikia wakati wa mahojiano hayo alikuwa bado hajamweleza mtoto mdogo kuhusu kifo cha mama yao

Muhtasari

•Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alifichua kwamba amekuwa kwenye ndoa na marehemu Wambui kwa takriban miaka 30.

•Alipoulizwa kwa nini amekuwa akihifadhi habari za familia yake, Makokha alisema, "Hayo ni maelezo yangu ya kibinafsi."

Alphose Makokha
Image: HISANI

Muigizaji na mchekeshaji mkongwe wa Kenya Matayo Kenya almaarufu Alphonse Makacha Makokha amefichua baadhi ya mambo kuhusu familia yake na kuhusu marehemu mkewe Purity Wambui.

Katika mahojiano na Tuko Kenya, muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alifichua kwamba amekuwa kwenye ndoa na marehemu Wambui kwa takriban miaka 30.

Alikataa kutaja idadi kamili ya watoto wao lakini akadokeza kuwa ni wengi.

“Kikwetu huwa hatuhesabu watoto. Watoto ni wengi,” Makokha alisema.

Muigizaji huyo mcheshi pia alizungumzia jinsi watoto wake wanavyopambana na majonzi kufuatia kifo cha mama yao mapema mwezi huu.

Alisema kuwa kufikia wakati wa mahojiano hayo alikuwa bado hajamweleza mtoto mdogo kuhusu kifo cha mama yao kwani alitaka kwanza ampe ushauri nasaha.

“Watoto wako salama. Pia imewahit kwa sababu pia wao hawaamini. Imewahit. Mdogo zaidi ana miaka 11. Imemuathiri kwa sababu huyo mdogo anauliza kila wakati mama yuko wapi. Unajua lazima nimpatie ushauri nasaha pia, lakini ukweli ni kwamba lazima nitamwambia mama hatuko naye tena, ameenda kwa Mungu,” alisema.

Alipoulizwa kwa nini amekuwa akihifadhi habari za familia yake, Makokha alisema, "Hayo ni maelezo yangu ya kibinafsi."

Muigizaji huyo mkongwe hata hivyo alibainisha kuwa amekuwa akisaidia familia yake kila wakati.

“Kuwasupport nimewasupport kabisa. Hiyo ndiyo ukweli wa mambo. Kuwasupport nimewasupport, hakuna siku kumekuwa na shida yoyote. Wako sawa,” alisema.

Mke wa Makokha, marehemu Purity Wambui alipoteza maisha mnamo Juni 1, 2024 baada ya kuugua saratani ya matiti kwa muda mrefu.

Muigizaji huyo mkongwe alifichua kuwa mkewe alifariki akiwa nyumbani. Alisema kuwa marehemu alikuwa chini ya uangalizi wa binti yao wakati alifariki.

“Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa nimewacha binti yangu nikamwambia amuangalie mama yake, naenda kutafuta riziki,” alisimulia.

Alifichua kuwa ni muigizaji mwenzake Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ambaye alifahamishwa wa mara ya kwanza kuhusu kufariki kwa mkewe.

Ondiek kisha akamjulisha kuhusu habari hizo za kusikitisha kwa njia ya huruma.

“Nililia kwa muda wa saa mbili hivi. Mimi ndiye nilikuwa nikiendesha gari, yeye (Ondiek) alichukua usukani na kuendesha. Nikasema kwa sababu imefanyika, tuendelee na safari. Nikaenda kazini tu kama kawaida. Hiyo siku tulikuwa tulale lakini ata sikulala, lazima ningerudi. Mungu alinipatia nguvu nikawapeleka nyumbani vizuri, pia mimi nikafika nyumbani vizuri,” alisema.

Makokha alisema kuwa baada ya kufika nyumbani jioni hiyo, alikuwa na usiku mbaya kwani alilia sana hadi mida ya asubuhi.

Muigizaji huyo alisema tayari anakosa kelele ambazo mkewe alikuwa akimpigia nyumbani.