YouTube ya msanii Diana B yadukuliwa, mdukuzi abadilisha jina

Muhtasari

• Mwanamuziki huyo chipukia ambaye pia ni mkewe Bahati amedai kuwa mdukuzi amefuta jina lake (Diana) na kutundika jina lake kwa akaunti hiyo.

• Mwaka jana msanii Bahati alimzindua rasmi mke wake Diana Marua kama msanii na kumbandika jina la usanii Diana B.

 

Diana Marua
Diana Marua
Image: hisani

Akaunti ya YouTube ya Diana B imedukuliwa. Mwanamuziki huyo chipukia ambaye pia ni mkewe Bahati amedai kuwa mdukuzi amefuta jina lake (Diana) na kutundika jina lake kwa akaunti hiyo. 

Mwaka jana msanii Bahati alimzindua rasmi mke wake Diana Marua kama msanii na kumbandika jina la usanii Diana B.

Katika ngoma zake mbili za kwanza, mashabiki wengi walikuwa na maoni mbali mbali kuhusu kipaji chake na iwapo atastahimili uzito wa sekta hii iliyojaa shinikizo za aina yake.

Mwaka huu (2022) ulipoanza wengi wamekuwa wakisubiri kazi nyingine kutoka kwake Diana B, huku Bahati akitoa ishara kupitia ukurasa wake wa Instagram kwamba ngoma ya kwanza kutoka kwa msanii huyo ingeshuka kwenye mtandao wa youtube tarehe 26/01/2022.

Lakini sasa kwa jinsi hali ilivyo, mashabiki watatakikana kusubiri kwa muda  zaidi ili kupokea kazi kutoka kwake Diana B, hii ni baada ya kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram jana kwamba akaunti yake ya Youtube imedukuliwa na watu wasiojulikana.

Diana B aliongeza kwamba amejituma sana kuhakikisha anajenga uhusiano mzuri baina yake na wasanii wengine na kwa hivyo hajui mbona mtu angefikiria kumfanyia kitendo kama hicho.

"Nimeishi kwa amani na Kila mtu na siku zote nimekaa kwenye njia yangu; sijui Kwa nini mtu yeyote atanifanyia hivi! UnaHack Akaunti Yangu ya YouTube; Unabadilisha jina na mbaya zaidi  unafuta jina langu,"

Licha ya kuwa ni kitendo ambacho hakiwezi kushabikiwa na mtu yeyote, kuna wale wanahisi kwamba familia hii yenye wasanii wawili inajaribu kujenga' kiki' ili kusukuma mziki wao na kusajili idadi kubwa ya mashabiki wanaofuatilia kazi zao kwenye mitandao ya kijamii. Hii inatokea kwa kuwa mwaka juzi, Bahati na Diana B walionekana kutofuatiliana kwenye mitandao na hata kufuta picha walizopiga pamoja kwenye mtandao wa Instagram. Hali kama hii imeleta sintofahamu miongoni mwa mashabiki huku wakikosa imani na baadhi ya wasanii wanaojenga vipaji na sanaa zao kupitia 'kiki'.

Diana B ameongeza kwamba usimamizi wake upo kwenye mazungumzo na Youtube ili kuhakikisha kwamba wanafahamu aliyekuwa nyuma ya kitendo hicho, huku akiwasihi mashabiki wake wawe watulivu na wazidi kufuatilia mtandao wake wa Instagram ili kupata maelekezo zaidi.