Killy apasua mbarika sababu zilizomfanya kuondoka lebo ya Alikiba

Muhtasari

• Killy alieleza changamoto alizokumbana nazo kabla ya kusajiliwa na Lebo ya Konde Gang ambayo kwa sasa inafanya vyema  kanda ya Afrika mashariki na Afrika nzima.

•Killy ambaye  amekuwa  humu nchini , kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari alieleza changamoto alizokumbana nazo kabla ya kusajiliwa na Lebo ya Konde Gang ambayo inaendelea kufanya vyema kanda la Afrika Mashariki

msanii wa Konde Gang,Killy
msanii wa Konde Gang,Killy
Image: Hisani

Msanii kutoka nchini Tanzania, Killy ameeleza sababu zilizomfanya kuondoka lebo ya King Kiba ambayo inamilikiwa na nguli wa muziki wa Bongo Flavor Alikiba.

Killy ambaye  amekuwa  humu nchini, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari alieleza changamoto alizokumbana nazo kabla ya kusajiliwa na Lebo ya Konde Gang ambayo inaendelea kufanya vyema kanda ya Afrika Mashariki.

“Muziki una changamoto nyingi, kufika hapa nilipo imekuwa si rahisi, mimi ni msanii mkubwa na ninahisi natakiwa kuwa kwenye record label kubwa, lakini sijasema lebo ya Alikiba si kubwa,"alisema Killy.

Killy ambaye anajulikana sana na wimbo 'wewe' aliiendelea kusema kutoka kitambo wamekuwa na mawasiliano mema na Harmonize hivyo wakati aliamua kuondoka  kwenye lebo ya Alikiba hakuwa na shaka ya kujiunga na lebo ya Konde Gang kuendeleza kazi yake ya muziki. 

Vilevile, alidokeza kuwa hakuwa na mkataba wowote na lebo ya Alikiba hivyo  ilikuwa rahisi kuondoka kwenye lebo hiyo.  

"Kule kwa Kiba sikuwa na mkataba kwa hivyo ilikuwa rahisi kwangu kuondoka, kwanza nilipumzika nifikirie hatua nyingine ya kuchukua kabla sijaamua kutulia kwenye lebo  ya Harmonize, Mimi na Alikiba bado tuko kwenye mahusiano mazuri na bado huwa tunazungumza." Alieleza.