"Tuko sawa" Eric Omondi azungumzia uhusiano wake wa sasa na Jacque Maribe

Muhtasari

•Omondi alisema kwa sasa uhusiano wake na Bi Maribe ni mzuri kufuatia mazungumzo mazuri ambayo walishiriki mwaka jana.

•Alitangaza kwamba anakusudia kufunga ndoa na mpenzi kutoka nje ya Afrika kufuatia majaribio kadhaa yasiyozaa matunda na wanadada wa hapa barani.

Jackie Maribe na Eric Omondi walipopatana siku ya Alhamisi
Jackie Maribe na Eric Omondi walipopatana siku ya Alhamisi
Image: SIMON KABU

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amesema kwa sasa hakuna uhasama wowote kati yake na baby mama wake Jacque Maribe.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Omondi alisema kwa sasa uhusiano wake na Bi Maribe ni mzuri kufuatia mazungumzo mazuri ambayo walishiriki mwaka jana.

Omondi ambaye anaaminika kuwa baba ya mtoto wa mtangazaji huyo alisema ingawa hawakurejesha mahusiano ya kimapenzi, wao ni marafiki.

"Tulikutana, tukazungumza na kukubaliana. Kwa sasa sisi ni marafiki. Tuko sawa mimi na Jacque" Eric alisema.

Mchekeshaji huyo hata hivyo aliweka wazi kwamba hatakuwa anaonyesha upendo wake kwa mzazi huyo mwenza katika msimu huu wa Valentines kwa kuwa tayari ana mpenzi mwingine.

Eric pia alitangaza kwamba anakusudia kufunga ndoa na mpenzi kutoka nje ya Afrika kufuatia majaribio kadhaa yasiyozaa matunda na wanadada wa hapa barani.

"Sitaki bibi Mwafrika. Nataka mzungu, mwarabu ama Mchina. Nikipata mchinku itakuwa nzuri zaidi" Eric alisema.

Eric anajulikana kuwahi kuwa katika mahusiano yasiyofanikiwa na wanawake kadhaa  ikiwemo Jackie Maribe, Chantal Grazioli kati ya wengineo.