Pesa ni Zake! Video ya Mulamwah yazua mjadala mitandaoni

Muhtasari

• Mchekeshaji maarufu nchini Kendrick Mulamwah amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya kuonekana kwenye instastories zake akihesabu bunda la noti

• Mashabiki wake wengi mitandaoni wamechanganyikiwa na kitendo hiki huku maoni kinzani yakigubika video yenyewe.

Mulamwah
Image: Facebook

Mchekeshaji maarufu nchini Kendrick Mulamwah amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya kuonekana kwenye instastories zake akihesabu bunda la noti, kima kinachodhaniwa kuwa takribani milioni moja na laki mbili, pesa taslimu.

Katika video hizo, Mulamwah anaonekana akihesabu na kukagua pesa hizo nje chini ya kivuli cha migomba huku akijiburudisha na githeri.

Mashabiki wake wengi mitandaoni wamechanganyikiwa na kitendo hiki huku maoni kinzani yakigubika video yenyewe.

Baadhi ya mashabiki wake wanasema anahatarisha utajiri wake kwani kitendo cha kuonesha pesa kiasi hicho tena hadharani kinaweza msababishia kuvamiwa na wahuni na kumpora kiasi hicho.

Wengine wanasema  ni haki yake kujianika kwenye mitandao kwani pesa ni zake na ana kila haki na sababu ya kuringa nazo kwa sababu anajua alizipata kwa njia halali.

Mulamwah aligonga vichwa vya Habari mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuvunja mahusiano na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonia na kisha baadae chini ya saa mbili akaibuka mitandaoni na picha ya mwanadada aliyemtaja kama chaguo mbadala kwa Sonia.