Marioo aihama Simba, atoa wimbo kuishabikia Yanga

Muhtasari

• Msanii wa kizazi kipya Marioo ametangaza kuhama timu ya Simba na kujiunga ushabiki na mahasidi Yanga, na kutoa wimbo wa kuisifia timu yake mpya.

Marioo
Image: Facebook

Msanii wa kizazi kipya Marioo ametangaza kuhama timu ya Simba na sasa atashabikia mahasidi wao Yanga, na kutoa wimbo wa kuisifia timu yake mpya.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa shabiki wa timu ya Simba mpaka hata kushiriki katika tamasha zao mbali mbali kama Simba Day amechukua uamuzi wa kuihama timu hiyo na kuanza kushabikia Yanga kwa kile alikitaja kwamba Simba inamsababishia msongo wa mawazo, kitu ambacho hakitaki.

Marioo ambaye amedondosha kibao kipya cha kuisifia Yanga Februari 21, na amekipa jina Yanga Tamu amesema kwamba ni mwanzo mpya na kuwataka mashabiki wake kusherehekea ufanisi wa Yanga na wimbo huo mpya.

“Tumeutoa wimbo wetu mpya ambao ni Yanga Tamu, kila mmoja ameona jinsi ambavyo Yanga imekuwa tamu siku zote na itaendelea kuwa tamu, that’s why tukaona iwe hivo. Sasa nipo rasmi Yanga, zamani nilikuwa nashabikia timu ile nyingine. Mimi sipendi stress, tuenjoy na wimbo huu wa Yanga tamu,” amesema Marioo katika uzinduzi wa kibao hicho na wanakamati wa timu ya Yanga.

Mwanzoni mwa msimu huu, pia aliyekuwa msemaji wa timu ya Simba Haji Manara aligura timu hiyo na kufuata mkondo huo huo ambapo alijiunga na Yanga kama msemaji wao mpya na ambapo kazi yake imeisaidia timu ya Yanga kuhimili ushindani mkali na katika msimamo wa ligi mpaka sasa.

Timu ya Yanga inazidi kudedea kileleni mwa jedwali la NBC nchini Tanzania ikifuatiwa kwa umbali na mahasidi wao wa tangu jadi, Simba SC.