Jimal Rohosafi azungumzia suala la Amber Ray kufuta tattoo ya jina lake

Muhtasari

•Jimal aliweka wazi kuwa hakumshinikiza mwanasoshalaiti huyo kuweka wala kufuta tattoo hiyo.

•Alisema kwa sasa amechoshwa na mahusiano na kuapa kuwa atajipatia muda wa angalau miaka mitatu kabla ya kusaka kipenzi kipya.

Amber Ray na Jimal Rohosafi
Amber Ray na Jimal Rohosafi
Image: INSTAGRAM

Mfanyibiashara mashuhuri jijini Nairobi Jimal Rohosafi amefunguka suala la aliyekuwa mpenzi wake Amber Ray kufuta tattoo ya jina lake.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Jimal aliweka wazi kuwa hakumshinikiza mwanasoshalaiti huyo kuchorwa wala kufuta tattoo hiyo.

Baba huyo wa watoto wawili alifichua kwamba ilikuwa ndoto ya Amber Ray kuchorwa tattoo ya jina lake kwa kuwa alikuwa amezama kwenye huba lao.

"Ilikuwa ndoto yake. Aliniambia kuwa akipenda mtu basi anampenda asilimia 100. Hiyo ilikuwa ndoto yake kuweka tattoo. Hatua ya kuifuta pia ni chagua lake," Alisema.

Jimal alifichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa tattoo ila mwenyewe hana mchoro wowote kwenye mwili wake.

Mfanyibiashara huyo pia alisisitiza kuwa alijitolea 100% katika mahusiano yake ya hapo awali licha ya kuwa hayakufua dafu. Alisema kwa sasa amechoshwa na mahusiano na kuapa kuwa atajipatia muda wa angalau miaka mitatu kabla ya kusaka kipenzi kipya.

"Mimi hujitolea sana katika mahusiano. Nikiamua kupenda, napenda. Huwa sirudi nyuma, najipeana mzima mzima. Shida hutokea wakati naanza kurudi nyuma. Ndio maana nikasema mahusiano sio yangu. Nikiamua kujitosa kwenye mahusiano hiyo itakuwa baada ya miaka mitatu na mara moja nitaingia kwa ndoa. Kwa sasa nimeoa biashara yangu," Alisema.

Mwaka uliopita mwenyekiti huyo wa muungano wa wamiliki matatu jijini Nairobi  aliangaziwa sana mitandaoni kufuatia masaibu yaliyokuwa yamekumba ndoa yake.

Mahusiano yaliyofeli ya Jimal na Amber Ray yalipelekea kutengana kwake na mkewe na mama ya wanawe wawili, Amira.