"Niko single!" Amira athibitisha kutengana na mfanyibiashara Jimal Rohosafi

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto wawili amesisitiza kuwa kwa sasa hategemei jasho la mwanamume yeyote na kile anachopata kinatokana na bidii yake.

Amira na aliyekuwa mumewe Jimal Rohosafi
Amira na aliyekuwa mumewe Jimal Rohosafi
Image: INSTAGRAM//

Mjasiriamali Amira na ambaye alikuwa mke wa mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu jijini Nairobi Jimal Marlow Rohosafi amethibitisha kwamba ndoa yao iligonga mwamba.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Amira ameweka wazi kwamba kwa sasa hana mchumba na  anajitegemea mwenyewe.

Mama huyo wa watoto wawili amesisitiza kuwa kwa sasa hategemei jasho la mwanamume yeyote na kile anachopata kinatokana na bidii yake.

"Siku nyingine tu ya kukukumbusha kuwa sina mchumba na ninatia bidii kubwa kupata mali yangu mwenyewe" Amira amesema.

Haya yanajiri takriban miezi miwili baada ya malkia huyo kudai talaka kutoka kwa aliyekuwa mume wake Jimal Rohosafi.

Amira alionekana kukerwa na uhusiano kati ya mume wake na mwanasoshalaiti Amber Ray na kudai kuwa hangeweza kuvumilia katika ndoa hiyo.

Ni hatua ambayo nilifaa kupiga kitambo lakini sikuwa na ujasiri. Lakini inafika wakati  ambapo unasema imetosha! Leo nimefika mwisho, natumai hatua hii itawapatia wengine ujasiri wa kuacha yale ambayo yanawavuta nyuma. Nafanya juhudi kuwa bora na kuangalia watoto wangu, na kufanya biashara yangu. Hatua moja kwa wakati" Amira alisema mnamo mwezi Novemba.

Baadaye Amira alionekana katika mahakama ya Kadhi ambako aliwasilisha ombi la kumtaliki mfanyibiashara huyo.