Kuachana hakujawahi kunifanya niogope kupenda tena- Vera Sidika azungumzia mahusiano yake

Muhtasari

•Vera amedai kuwa kuvunjika kwa mahusiano hakujawahi kumzuia kujitosa kwenye mahusiano mapya.

•Vera pia amepuuzilia mbali ugomvi na mwanasoshalaiti mwenzake Amber Ray huku akidai kuwa hazozani na mtu yeyote yule.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti Vera Sidika amekiri kuwa dhiki za mahusiano yake ya awali hazijawahi kumtia hofu ya kupenda tena.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amedai kuwa kuvunjika kwa mahusiano hakujawahi kumzuia kujitosa kwenye mahusiano mapya.

"Sijawahi kuogopa kupenda tena. Maisha yanasonga mbele na kuwa bora tu," Vera alisema alipokuwa anashirikisha mashabiki wake katika kipindi  cha maswali na majibu.

Vera amedai kuwa Brown Mauzo ni bora zaidi kuliko wanaume wengine ambao amewahi kuchumbia hapo awali.

"Yeye ni mkubwa zaidi kuliko wote ambao nimewahi kichumbia na sikuamua kuwa mjamzito. Tuko kwenye ndoa na tunapendana sana. Yeye ni bwana yangu na baba ya binti yetu mrembo, Asia," Vera alijibu shabiki aliyetaka kujua mbona aliamua kupata mtoto na Mauzo licha ya kuchumbia watu wengine "wakubwa" hapo awali.

Mama huyo wa binti mmoja amejitokeza mara nyingi kujigamba kuhusiana na mahusiano yake ya sasa na mwanamuziki Brown Mauzo. Ameonekana kujivunia ndoa yao ya takriban mwaka mmoja unusu.

Mnamo siku ya Valentines Vera alimtaja mumewe kama mwanaume bora zaidi kuwahi kuwa katika  maisha yake.

"Siku hii ya wapendanao ni ya pekee zaidi kwa sababu ninapata kuisherehekea pamoja na mtoto wangu Asia na mwanamume mzuri zaidi kuwahi kutembea duniani na anayejali Brown Mauzo maneno hayawezi kuelezea upendo wangu kwako na kwa familia yetu ndogo ya kupendeza. Umekuwa baba bora zaidi kwa binti yetu na uthibitisho kwamba wanaume wazuri bado wapo. Heri za siku ya wapendanao kwa mapigo ya wapenzi wangu Brown Mauzo na Asia Brown. Nawapenda nyote.Kwa kweli, mwaka jana siku kama hii Asia alikuwa akiogelea kuelekea tumboni mwangu" Vera alisema.

Hapo awali Vera amewahi kuwa kwenye mahusiano na watu kadhaa mashuhuri wakiwemo mwanamuziki Otile Brown, daktari Jimmy Chansa kutoka Tanzania na Yommy Johnson kutoka Nigeria.

Mahusiano ya Vera na Otile Brown yaligonga mwamba mwaka wa 2018 baada yao kuchumbiana kwa kipindi kifupi. Wawili hao walilaumiana kufuatia kuvunjika kwa mahusiano yao.

Katika kipindi hicho cha Q&A Vera pia amepuuzilia mbali ugomvi na mwanasoshalaiti mwenzake Amber Ray huku akidai kuwa hazozani na mtu yeyote yule.