Mhubiri James Ng'ang'a awakemea vijana wanaoeneza maneno machafu kumhusu

Muhtasari

•Ng'ang'a amesema vijana wadogo wanapaswa kuchunga maneno au habari wanazoeneza kuhusu wazee wao.

•Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 69 aliwakashifu wanavlogu ambao wamekuwa wakieneza habari tatanishi kumhusu.

Muhubiri James Ng'ang'a
Image: WILFRED NYANGARESI

Mhubiri James Maina Ng'ang'a wa Neno Evangelism Centre ameshtumu kizazi cha kisasa kwa kukosa heshima kwa wazee.

Mtumishi huyo wa Mungu aliyezingirwa na utata mwingi amedai kwamba kizazi hiki hakioni aibu kutumia maneno machafu dhidi ya wazee wao.

Ng'ang'a amesema vijana wadogo wanapaswa kuchunga maneno au habari wanazoeneza kuhusu wazee wao.

"Vijana wamekosa heshima kwa Mungu, kwa wazazi wenu na kwa watumishi wa Mungu. Hiyo ndiyo inaleta ugomvi.. Hata kama ni habari za ukweli, kuna mambo ambayo huwezi kusema kuhusu mzazi wako. Watu wa siku hizi hawana heshima, utasikia mtu akizungumza kuhusu mpenzi wa mzazi wake. Hayo ni maneno ya uchi," Ng'ang'a alisema kwenye mahojiano na Mpasho.

Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 69 pia aliwakashifu wanavlogu ambao wamekuwa wakieneza habari tatanishi kumhusu.

"Nimefanya mambo mingi. Ukija leo hii uandike karatasi ili uuze, hata hunisaidii ili watu wanipende ni kunichafua tu. Hiyo haiwezi kukusaidia. Unapigana na kile Mungu amechagua," Alisema.

Ng'ang'a aliweka wazi kwamba hajawahi kufanya chochote ili avume mitandaoni. Alisema kwamba watu wamekuwa wakimukuu vibaya kwa manufaa yao.

"Sikuwahi fanya kitu ili nivume. Ni watu wanakata mahali nimeongea. Hawataki kuchunguza mbona nimesema kitu. Hawataki kuangalia mbele na mwanzo. Wanakata tu mahali tatanishi nakuweka hiyo," Alisema.

Mhubiri huyo hata hivyo alisema maneno hasi kumhusu ambayo huenezwa mitandaoni huwa hayamwathiri kwani badala ya kumshusha huwa yanamjengea umaarufu zaidi.