"Wasichana hawataki kuangalia uzee!" Pastor Ng'ang'a azungumzia jinsi amekuwa akitongozwa

Muhtasari
  • Mhubiri huyo mwenye miaka 69 alisema wanawake wamekuwa wakimtongoza bila kujali umri wake mkubwa wala kutawazwa kwake.
  • Mhubiri huyo mcheshi aliwatahadharisha wanawake dhidi ya kutumia jumbe wanazoona kwa simu zao waume zao kupima uaminifu wao. 
Mhubiri James Nganga akitoa hotuba katika harusi ya bintiye mnamo Machi 19, 2022
Image: WILFRED NYANGARESI

Mhubiri aliyezingirwa na utata mwingi, James Ng'ang'a wa Neno Evangelism Centre amefichua kwamba amekuwa akipokea jumbe kochokocho za kimapenzi kwenye simu yake kutoka kwa wanadada wanaommezea mate.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mhubiri huyo mwenye miaka 69 alisema wanawake wamekuwa wakimtongoza bila kujali umri wake mkubwa wala kutawazwa kwake.

Ng'ang'a alisema mapenzi ya kweli hayapo tena siku hizi huku akidai kuwa wanawake wa siku hizi wanalenga pesa badala ya mapenzi.

"Namba yangu ina watu zaidi ya 1000. Huwa natumiwa jumbe na mafuta hii yote. Wasichana hawataki kuangalia uzee. Wanatuma jumbe wakisema nakaa vizuri, mimi ni mtanashati. Huwezi kosa kuchokozwa ukiwa mtu mashuhuri," Ng'ang'a alisema.

Mhubiri huyo mcheshi aliwatahadharisha wanawake dhidi ya kutumia jumbe wanazoona kwa simu za waume zao kupima uaminifu wao. 

Kulingana na Ng'ang'a , wanaume hawafai kuhukumiwa kutokana na jumbe wanazopokea kwa simu zao kwani huo sio ushahidi tosha kuwa wanaenda nje ya ndoa.

"Mumeo akitaka kufanya chochote atafanya na hutajua. Ukiamini jumbe pekee basi umekosea maana mchana ameshinda mwenyewe na huwezi ukajua. Kama hutamuamini basi ata kuangalia jumbe ni kazi ya bure. Kina mama waache kutegemea jumbe," Ng'ang'a alisema.

Ng'ang'a pia aliwasihi wanawake kuwalinda mabwana zao huko akiwaonya kuwa kuna wanawake wengine wengi wanaosubiri ndoa zao zivunjike ili wachukue nafasi zao.