Pastor Ng'ang'a afunguka kuhusu maisha yake ya uhalifu yaliyompelekea kufungwa miaka 20

Muhtasari

•Mhubiri huyo aliyezingirwa na utata mwingi katika taaluma yake alifichua kwamba aliwahi kuhudumu kifungo cha jela cha miaka ishirini.

•Ng'ang'a  alisisistiza kwamba imeshikilia imani yake tangu alipofanya maamuzi ya kuokoka akiwa gerezani.

Askofu David Ng'ang'a
Askofu David Ng'ang'a
Image: IVY MUTHONI

Mhubiri mashuhuri nchini James Ng'ang'a wa Neno Evangelism Centre amekiri kwamba historia ya maisha yake sio ya kusifiwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mhubiri huyo aliyezingirwa na utata mwingi katika taaluma yake alifichua kwamba aliwahi kuhudumu kifungo cha jela cha miaka ishirini.

Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 69 alisema alijipata gerezani baada ya kushtakiwa kwa makosa tofauti tofauti ya uhalifu.

"Nilikuwa jambazi, nilikuwa na bunduki, nilikuwa naiba, nilikuwa napigana. Hayo yote nilifanya. Siku moja niliskia injili na nikatamani. Nilisikia mtu akisema kuna kuokoka nikainua mkono na kuokoka. Nilihubiri gerezani miaka miwili," Ng'ang'a alisimulia.

Mtumishi huyo wa Mungu alifichua kwamba aliachiliwa huru mnamo mwaka wa 1992. Alisema kwamba imeshikilia imani yake tangu kuokoka kwake akiwa gerezani.

"Mimi sio kama wahubiri wengine. Nimekaa gerezani miaka 20. Nimevuta bangi, nimekunywa pombe, nimeiba, nimeshikwa na bunduki kisha nikaokoka. Niko na ujuzi ambao hao wengine hawana," Alisema.

Ng'ang'a pia alifichua kwamba aliwahi kufanya kazi nyingi za mkono kabla ya kujizolea utajiri ziliwemo kuuza maembe, kubebea watu mizigo na zinginezo.