Mhubiri James Ng'ang'a aeleza sababu zake kutojua idadi halisi ya watoto wake wengi

Muhtasari

•Ng'ang'a alikiri kuwa alishiriki mapenzi na wanadada wengi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ambacho aliishi maisha ya uasherati.

•Mhubiri huyo alifichua kwamba alianza kupata watoto na wanawake tofauti akiwa na umri mdogo.

Mhubiri James Nganga akitoa hotuba katika harusi ya bintiye mnamo Machi 19, 2022
Image: WILFRED NYANGARESI

Mhubiri mwenye utata mwingi  James Maina Ng'ang'a wa Neno Evangelism Centre amekiri kuwa hana uhakika kuhusu idadi ya watoto na wajukuu alionao.

Akizungumza na Mpasho, Ng'ang'a alifichua kwamba alianza kupata watoto na wanawake tofauti akiwa na umri mdogo.

Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 69 alisema hana uhakika kuhusu idadi ya wanawake aliopata nao watoto kabla hajapiga hatua ya kuokoka.

"Nilianza kuzaa miaka mingi iliyopita. Nina watoto wengi. Sisi wanaume hatujui mtoto huwa wa nani. Wamama ndio wanaweza kutuambia ni wa nani. Siwezi jua ni wangapi kwa sababu siko kortini. Siwezi kujua hata idadi ya wajukuu kwa sababu niliishi zaidi ya miaka 25 bila mpango," Ng'ang'a alisema.

Ng'ang'a alikiri kuwa alishiriki mapenzi na wanadada wengi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ambacho alikuwa mwathiriwa wa uasherati.

Alifichua kuwa aliyekuwa mke wake wa kwanza aligura ndoa akiwa na ujauzito wa mapacha. 

"Hatukuwa tumeoana rasmi, tuliishi pamoja tu. Alienda kuchukua nguo kwao akiwa mjamzito ila hakurudi. Nilipookoka nilimwendea kwao nikakuta amejanjaruka, akaniambia hatukuwa tumeoana rasmi niende zangu. Baadaye aliaga kisha watoto wakaja kunitafuta," Alisimulia.

Mhubiri huyo alifunga pingu za maisha na mkewe wa sasa, Mercy Murugi takriban mwongo mmoja uliopita.