"Inanikwaza sikuwahi kukuambia nakupenda kabla kuaga" Otile Brown amkumbuka marehemu mamake

Muhtasari

•Otile Brown alimsherehekea mzazi huyo wake ambaye aliaga takriban miaka 16 iliyopita kwa kuchangia mafinikio yake makubwa ya sasa.

•Baada ya kifo cha mamake, Otile Brown alichukuliwa na nyanya yake ambaye alijaribu kujaza pengo lililoachwa.

Image: INSTAGRAM// OTILE BROWN

Mwanamuziki Jacob Obunga almaarufu Otile Brown alimkumbuka marehemu mama yake wikendi ambayo imetamatika.

Otile Brown alimsherehekea mzazi huyo wake ambaye aliaga takriban miaka 16 iliyopita kwa kuchangia mafinikio yake makubwa ya sasa.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 30 hata hivyo alisema anajuta sana kutowahi pata fursa ya kumwambia mamake jinsi alivyompenda kabla ya kifo chake.

"Marehemu mama. Shukran kwa kunifanya mwanaume niliye sasa. Inanikwaza sikuwahi kukuambia nakupenda kabla kuaga dunia," Otile alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Otile Brown aliambatanisha ujumbe wake na wimbo ambao alitengeneza maalum kwa mzazi huyo wake.

"Inanikwaza sikuwahi kukuambia nakupenda kabla uondoke. Na inanichoma moyo wangu, inaikwaza nafsi yangu maana sikupata muda mama yangu.." Wimbo huo wake ulisema.

Hapo awali Otile Brown aliwahi kufichua kuwa mama yake aliaga dunia mwaka wa 2006. Wakati  huo Brown ambaye ndiye kifunga mimba katika familia yao alikuwa na umri wa miaka 14 tu.

Baada ya kifo cha mamake, Otile Brown alichukuliwa na nyanya yake ambaye alijaribu kujaza pengo lililoachwa.