Hatupaswi kamwe kuhisi vibaya kuhusu kuzeeka- Esther Musila awashauri wanawake

Muhtasari

•Musila aliwadokezea wanawake wa rika lake kuwa kutimiza umri mkubwa waliotimiza ni fursa maalum ambayo wanapaswa kukumbatia. 

•Musila alifunga pingu za maisha na Guardian Angel mapema mwaka huu licha ya kuwa amemzidi umri msanii huyo kwa takriban miaka 20.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Image: INSTAGRAM//GUARDIAN ANGEL

Bi Esther Musila amewataka wanawake waliopiku umri wa miaka 40 kujikubali na kukumbatia uzee kadri unavyonyemelea.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, Musila aliwadokezea wanawake wa rika lake kuwa kufikisha umri mkubwa waliotimiza ni fursa maalum ambayo wanapaswa kukumbatia. 

"Hata kama miili yetu haiwezi kuwa kama ilivyokuwa hapo awali, inabeba roho zetu, ujasiri wetu, na nguvu zetu. Hatupaswi kamwe kuhisi vibaya kuhusu uzee. Ni upendeleo ambao umenyimwa kwa wengi. Furahia kila dakika," Musila alisema.

Mke huyo wa mwanamuziki Guardian Angel amewasihi wanawake kukumbatia mabadiliko katika miili yao. Vilevile amewataja wanawake hao kama mashujaa kwa kuwa tayari wametimiza mengi katika maisha yao.

Tuko katika umri ambapo tunaona makunyanzi, mvi na kilo zaidi. Tumeendesha kaya, tumelipa bili, tumeshughulikia magonjwa, huzuni, na kila kitu kingine ambacho maisha yametupangia. Sisi ni waathirika . Sisi ni mashujaa tulionyamaza," Alisema.

Licha ya kutimiza miaka 52 tayari, Bi Musila anaishi maisha ambayo wanadada wengi wenye umri wa ujana wanayatamani.

Musila alifunga pingu za maisha na Guardian Angel mapema mwaka huu licha ya kuwa amemzidi umri msanii huyo kwa takriban miaka 20.