Mwanaume apambana na Simba mpaka kumuua kwa mikono mitupu, bila kutumia silaha

Muhtasari

• Mwanaume mmoja kutoka wilaya ya Ganga, mashariki mwa Uganda aligonga vichwa vya habari baada ya kumuua simba kwa mikono bila silaha.

Mwanaume Mganda aliyepambana na Simba hadi kumuuwa
Mwanaume Mganda aliyepambana na Simba hadi kumuuwa
Image: Maravi (facebook)

Mwanaume mmoja nchini Uganda kutoka Wilaya ya Ganga wikendi iliyopita aligonga vichwa vya habari na kuwa gumzo kubwa mitandaoni baada ya kusemekana kwamba alifanikiwa kumuuwa mnyama simba kwa mikono yake bila kutumia silaha baada ya mapambano ya muda mrefu nyumbani kwake.

Kulingana na picha zilizovujishwa mitandaoni, mwanaume huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi kutoka mashariki wa Uganda alikuwa nyumbani kwake wakati Simba alivizia.

Tofauti na wengi ambao wangechana mbuga kwa kutumia msemo maarufu wa miguu niponye, mwanaume huyo alipiga firimbi ya kutangaza vita baina yake na simba pasi na kutumia silaha yoyote.

Mapambano yalianza. Jamaa na simba wakapapurana. Wakajeruhiana na hatimaye mwanadamu akaibuka mshindi kwa kumlemea Simba baada ya kumshambulia vikali tena kwa mfululizo mpaka kufa.

Mwanaume huyo aliyefananishwa na hadithi ya Samson katika Biblia takatifu hata hivo alijeruhiwa vikali pia na simba huyo kwani haikuwa ngoma ya kitoto kwa kweli.

Wanaume wenzako wanapambana na Simba mpaka kumuua wewe hapo ukiona paka nywele zinakusimama na kuomba ardhi ipasuke na kukumeza!