"Tunashirikiana kikazi, mapenzi la!" Stivo asema baada ya kuonekana pamoja na ex wake klabuni

Muhtasari

•Stivo alisisitiza kuwa kwa sasa hana uhusiano wowote wa kimapenzi na mpenzi huyo wake wa zamani. 

•Vishy alitupilia mbali uwezekano wake kurudiana na mwanamuziki huyo huku akidai kuwa tofauti zao haziwezi kusuluhishwa.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Mwanamuziki maarufu nchini Stivo Simple Boy alitumbuiza klabuni kwa mara ya kwanza mwaka huu usiku wa Jumapili.

Stivo aliwasili katika klabu ya Loft Lounge, jijini Nairobi akiwa ameandamana na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy na kuzua shaka kubwa kuhusu kutengana kwao.

Wawili hao hata hivyo waliweka wazi kwamba walikuwa pamoja kwa minajili ya kikazi ila sio kama wapenzi.

"Tumepatana kwa sababu ya biashara. Kila mtu huwa na kazi zake za kufanya. Leo kwa sababu biashara ni moja tukaamua tupatane. Tutatumbuiza pamoja," Pritty Vishy alisema alipokuwa anahutubia waandishi wa habari.

Vishy alifichua kuwa hiyo ilikuwa mara yao ya kwanza baada ya mahusiano yao kugonga ukuta mapema mwaka huu.

Stivo alisisitiza kuwa kwa sasa hana uhusiano wowote wa kimapenzi na mpenzi huyo wake wa zamani. Alidokeza kuwa moyo wake tayari umetekwa na mwanadada mwingine ambaye atakuwa anatambulisha hivi karibuni.

"Purity tunashirikiana kikazi lakini kwa mapenzi, la! Mahari tayari imeenda kwa mwingine, hivi karibuni mtamuona," Alisema Stivo.

Vishy alipoulizwa kuhusu uamuzi wake kuendelea kumsapoti Stivo licha ya kutengana kwao  alisema lengo lake ni kufanikisha safari  ya muziki ya msanii huyo kutoka Kibra bila kujali kuhusu tofauti zao.

"Mimi ndio nilifichua habari za Stivo kuteseka. Haina haja nimuachie katikati baada ya kumsaidia kwa sababu tuko na tofauti zetu. Ndio maana nimejitokeza kumsapoti. Niliahidi kumsaidia katika hali zote" Alisema.

Kipusa huyo hata hivyo alitupilia mbali uwezekano wake kurudiana na mwanamuziki huyo huku akidai kuwa tofauti zao haziwezi kusuluhishwa.

Alisema kuwa tayari amesonga mbele na maisha yake na kutangaza  kuwa kwa sasa anatafuta mchumba mwingine.

Wapenzi hao wa zamani walitangaza kutengana kwao mwezi Machi huku Vishy akimshtumu Stivo kwa kumcheza na mwanadada mwingine.