Amerix - Ni afadhali mke hajasoma lakini mtiifu kuliko mke msomi mwenye dharau katika ndoa

Amerix alihoji kwamba ukielewa falsafa hiyo, utakuwa umeelewa kwa nini maprofesa hutalikiana na wake wenye taaluma na kuwaoa vijakazi

Muhtasari

• Kulingana na Amerix, mwanamke mwenye hajapitia elimu ya darasani ya kumwezesha kuwa na taaluma maalum huwa ni mtiifu sana kwenye ndoa 

Mkuza maudhui maarufu wa Twitter, Amerix
Image: Mpasho News

Amerix, jamaa maarufu kwenye mtandao wa Twitter ambaye alijulikana pakubwa kwa kutunga jumbe zinazotetea haki za wanaume sana tena ameibuka na jipya na kama ilivyo kawaida yake, amelenga wanawake wasomi kwa vijembe vyake vyenye ncha kali.

Amerix sasa anadai kwamba ni heri mwanaume kuoa mwanamke mwenye hajasoma lakini mtiifu kwenye ndoa kuliko kuoa mwanamke msomi mwenye taaluma mwenye mikogo na dharau katika ndoa.

Kulingana na Amerix, mwanamke mwenye hajapitia elimu ya darasani ya kumwezesha kuwa na taaluma maalum huwa ni mtiifu sana kwenye ndoa na anaweza akamfanyia mumewe kila kitu kwa kutii.

Kwa upande mwingine, Amerix alisema kwamba mwanamke msomi mwenye taaluma yake aghalabu huwa na madharau katika ndoa kiasi kwamba mwanaume anapomuitisha kitu mwanamke huyo humuonesha kwa mdomo huku akiwa amekwama kwa simu yake mtandaoni.

“Afadhali kuoa mwanamke mnyenyekevu asiyejua kusoma na kuandika kuliko mwanamke msomi asiye na adabu ambaye ukiomba kikombe cha chai baada ya siku ya uchovu anakuelekeza kwenye microwave kwa mdomo,” aliandika Amerix kwenye Twitter yake.

Mtetezi huyo wa haki za mtoto wa kiume alizidi kusema kwamba wale ambao kwa bahati mbaya wamejipata kwenye hali hiyo wanaelewa zaidi kisa cha profesa msomi mwenye digrii zake kumtaliki mkewe msomi na kisha kuchukua mfanyakazi wa ndani kama mbadala yake.

“Utaelewa kwa nini profesa aliachana na mke wake wa PhD na kuoa kijakazi,” Amerix aliandika kwa msisitizo.

Baadhi ya watu walifurika kwenye Twitter kutoa maoni yake kuhusu kauli hii ya Amerix ambapo wengi walionekana kukubaliana naye huku baadhi wakipingana naye vikali.

“Hata biblia inaunga mkono kauli yako Mwalimu. nanukuu.' Ni afadhali kula mboga katika nyumba ya amani kuliko kula maziwa na asali karibu na mwanamke mwenye kelele', mwisho wa nukuu.” Mmoja kwa jina la Okoth Achola aliandika.

“Sidhani hivyo. Hata wanawake wenye PhDs wanaweza kuwa watiifu, haswa ikiwa ubora wa kusaidiana ni wa juu. Hata wajakazi wanaweza kupotea! Sio kesi ya Samaki mmoja akioza mtungo mzima umeoza,” Mwingine kwa jina la Dk. Pat Kaltenacht alitofautiana naye.

Maoni yake ni yapi kuhusu kauli ya Amerix?